KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanikiwa kupata pointi moja ugenini baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mwadui katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Mwadui Complex leo mchana.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi saba na kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ikilingana kwa pointi na Mbao lakini ikiizidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, lakini ilishuhudiwa dakika zote 45 za kipindi cha kwanza zikimalizika kwa timu hizo kila upande kutoliona lango la mwenzake.

Kipindi cha pili Azam FC ilianza kwa kasi na kupata bao la uongozi dakika ya 55 lililofungwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, aliyepiga shuti la pembeni akimalizia pande safi alilopewa na winga, Ramadhan Singano ‘Messi’.

Mwadui ilifanikiwa kusawazisha kwa bao lililofungwa na winga Charles Ilanfya, dakika ya 55 na kufanya hadi dakika 90 zinamalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu.

Katika mchezo huo, ilishudiwa mabao mawili ya Azam FC yakikataliwa na waamuzi wasaidizi yaliyofungwa na Danny Lyanga, moja katika kila kipindi, la kwanza mwamuzi akidai ameotea na la pili kumsukuma mtu kabla ya kupiga kichwa.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka mjini Shinyanga kesho Jumamosi asubuhi tayari kuanza safari ya kuelekea mkoani Mara kukipiga na Biashara United, mtanange utakofanyika Uwanja wa Karume, mjini Musoma Septemba 19 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, David Mwantika, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Joseph Mahundi, Frank Domayo/Yahya Zayd dk 90, Danny Lyanga, Salum Abubakar, Ramadhan Singano/Idd Kipagwile dk 74