KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kipo tayari kupambana na Mwadui kesho Ijumaa baada ya kumaliza maandalizi ya mwisho leo mchana kwenye Uwanja wa Mwadui Complex.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Mwadui kuanzia saa 8.00 mchana, unatarajia kuwa wa kwanza kwa Azam FC kucheza ugenini msimu huu huku Mwadui ikicheza kwa mara ya kwanza nyumbani.

Wakati ukiwa mchezo wa kwanza ugenini, tayari Azam FC imeshacheza mechi mbili za ligi msimu huu ilizoanzia nyumbani Azam Complex ikishinda zote kwa kuzichapa Mbeya City (2-0) na Ndanda (3-0).

Matokeo hayo yameifanya kujikusanyia pointi sita katika nafasi ya pili kwenye msimamo ikizidiwa na Mbao yenye saba kileleni, ambayo imecheza mchezo mmoja zaidi ya matajiri hao.

Wachezaji wote wa Azam FC waliosafiri na timu wako fiti kuelekea mchezo huo, isipokuwa beki Abdallah Kheri, ambaye ni mgonjwa huku kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu, akisubiriwa kujiunga na wenzake muda wowote kuanzia kesho akitokea kwenye majukumu ya timu yake ya Taifa ya Zimbabwe ‘The Warriors’.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya mwisho leo, ameweka wazi kuwa amekiandaa kikosi chake kupata matokeo mazuri kesho kwa kuibuka ushindi.

“Ninajiamini kuwa tutapata matokeo mazuri, lakini kujiamini sio jambo pekee la kukupa uhakika, lakini wachezaji wanatakiwa kujiamini wao wenyewe kuwa wanaweza kushinda pia mechi za ugenini hilo ndio jambo la muhimu sana,” alisema.

Nafasi ya kileleni  

Ushindi wowote kwa Azam FC kesho utakuwa umeirejeshea nafasi yake ya kileleni ikifikisha pointi tisa, timu pekee zinazoweza kuishusha  baada ya mechi za kesho kama zikipata ushindi mnono kwenye mechi zao, ni Simba, Mtibwa Sugar na Stand United zenye sita nazo, lakini Mtibwa na Stand wakiwa wamecheza mechi moja zaidi.

Historia kiujumla TPL

Kihistoria kwenye mechi za ligi, Azam FC imekutana mara sita na Mwadui, ikiwa imeshinda jumla ya mechi tano na kutoka sare mchezo mmoja.

Katika mechi hizo sita, Azam FC imekutana mara tatu na Mwadui ugenini kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Azam FC ikifanikiwa kushinda mara mbili na sare moja iliyopatikana msimu uliopita ikiwa ni ya bao 1-1, bao la matajiri hao likifungwa na aliyekuwa nahodha wa timu hiyo Himid Mao ‘Ninja’, kwa njia ya mkwaju wa penalti.