KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC itaanza ziara yake ya kusaka pointi tisa kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, kwa kuelekea Shinyanga kesho Jumanne alfajiri tayari kuvaana na Mwadui ya huko.

Azam FC itakipiga na Mwadui kwenye Uwanja wa Mwadui Ijumaa hii saa 8.00 mchana, ambapo baada ya mchezo huo itakuwa na kibarua kingine Musoma kuvaana na Biashara United Septemba 19 kabla ya kuelekea jijini Mwanza kumenyana na Alliance Septemba 23.

Msafara wa Azam FC utaondoka na wachezaji wote waliokuwa fiti kikosini, wakiwemo nyota saba waliokuwa kwenye majukumu ya timu za Taifa, nahodha Agrey Moris na msaidizi wake, Frank Domayo, David Mwantika, Mudathir Yahya, Yahya Zayd waliokuwa Taifa Stars.

Wengine wawili ni kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu (Zimbabwe) na Nickolas Wadada (Uganda).

Kuelekea mechi hizo tatu, Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amesema kuwa amekipanga kikosi chake kwa ajili ya ushindi huku akidai atakuwa na siku mbili za kukiweka sawa kikosi chake kabla ya kucheza Ijumaa.

“Kila wakati ni jambo muhimu kucheza kwa lengo moja la ushindi na timu inayoonyesha njaa kwa ajili ushindi itapata ushindi hiyo ni rahisi kwenye mpira, mpira unategemea na uamuzi (wachezaji), bila shaka unatakiwa kufunga bao moja zaidi ya mpinzani wako, hiyo inamaanisha kuwa wewe utashinda mechi hiyo,” alisema.

Akizungumzia kuwakosa awali wachezaji wake saba waliokuwa timu za Taifa yake kama kutamuathiri kuelekea mechi ijayo, alisema: “Mimi sidhani hivyo, walikuwa kwenye mazoezi nasi katika maandalizi ya mwanzo mwa ligi, wamecheza mechi ngumu sana za kufuzu hawajapoteza mechi zao, hii inamaanisha kuwa watarudi na matumaini wakiwa na morali nzuri sana cha muhimu wanatakiwa waonyeshe ari walizoonyesha kwenye mechi za Kimataifa.”

Azam FC inaelekea kwenye mechi hizo ikiwa imeanza vema ligi, kwa kushinda mechi zake mbili za awali ikizifunga Mbeya City (2-0) na Ndanda (3-0), na kujisanyia pointi sita zinazoifanya kukaa nafasi ya pili kwenye ligi ikiwa nyuma ya Mbao iliyocheza mechi moja zaidi ikijikusanyia pointi saba.