KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imemaliza programu ya mechi za kirafiki baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Reha, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam leo asubuhi.

Huo ni mchezo wa tatu wa kirafiki kwa timu hiyo wakati huu Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) ikiwa imesimama kupisha mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.

Mechi mbili za awali za kirafiki ilipoteza mmoja dhidi ya Transit Camp (2-1) huku ikitoka suluhu na Arusha United (zamani Oljoro JKT), ambayo mwezi ujao itaanza harakati za kupambana kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Katika mchezo huo dhidi ya Reha, Azam FC ilijipatia mabao yake kupitia kwa Wazir Junior aliyefunga la kwanza akitumia uzembe wa mabeki likiwa ni la kusawazisha kwa timu yake huku Danny Lyanga, akitupia la pili.

Mshambuliaji wa Reha, Maliki Dachi, alifanikiwa kufunga mabao yote mawili kwa timu yake, moja katika kila kipindi cha mchezo huo, ambao ulikuwa mkali na wa aina yake, ambapo katika kikosi chao kuna wachezaji wanne waliowahi kupita Azam Academy.

Wachezaji hao ni beki Abbas Kapombe, aliyekuwa kwa mkopo kwenye timu hiyo sambamba na Ramadhan Mohamed ‘Ramaninho’ ambaye ni majeruhi, viungo Rajab Odasi pamoja na Uzoka Ugochukwu.

Mara baada ya mchezo huo, uliotumika na benchi la ufundi la Azam FC kuwapima wachezaji na kuwaweka fiti, kikosi cha mabingwa hao kinatarajia kurejea mazoezini kesho Jumatatu jioni kujiweka sawa na mechi tatu zijazo za ligi itakazocheza ugenini.

Azam FC katika mechi hizo, itaanza kukipiga na Mwadui (Septemba 14), Biashara United (Septemba 19) kabla ya kuifuata Alliance na kukipiga nayo Septemba 23 kwenye Uwanja wa Nyamagana, mkoani Mwanza.