TIMU ya Azam Veteran imeonesha kuwa imepania kutwaa ubingwa wa michuano ya Urafiki Cup iliyoanza jana, baada ya kuiwashia moto Mikocheni Veteran kwa kipigo cha mabao 5-1.

Azam Veteran iliyoanza na kasi ya nguvu, ilijipatia mabao yake kupitia kwa nahodha wa kikosi hicho ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’, aliyefunga mawili, Amir Kikwa na Thobias Silas, wakifunga moja kila mmoja huku jingine likiwa la kujifunga kwa Mikocheni.

Jumla ya timu nyingine tano zinashiriki michuano hiyo, ukiondoa Azam nyingine zinazoshiriki ni wenyeji Gymkhana Veteran, Mikocheni Veteran, Dar Veteran, Bin Slum Veteran na JMK Park Veteran.

Azam Veteran inayoundwa na mastaa wengine kama Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC, Nassor Idrissa ‘Father’, Meneja wa timu, Phillip Alando, inatarajia kucheza mchezo wa pili wa michuano hiyo dhidi ya Dar Veteran kwenye Uwanja wa Gymkhana Ijumaa ijayo saa 1.30 usiku.