TIMU ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Azam FC (Azam U-20) imeinyuka Reha bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex jana jioni.

Mchezo huo ulikuwa ni maalumu kwa ajili ya kikosi hicho chini ya Kocha Mkuu, Meja Mstaafu Abdul Mingange, kujiweka sawa kuelekea ligi ya vijana kwa klabu za Ligi Kuu inayotarajia kuanza hivi karibuni.

Bao pekee la ushindi limefungwa kwa njia ya mkwaju wa penalti na beki kisiki wa timu hiyo, Lusajo Mwaikenda, iliyotokana na mshambuliaji wa timu hiyo, Hamisi Ngoengo, kuangushwa ndani ya eneo la 18.

Kocha Mkuu wa timu kubwa ya Azam FC, Hans Van Der Pluijm, alihudhuria mchezo huo na kukaa benchi akiwa na lengo la kuwamulika wachezaji wa timu ndogo na kutoa ushauri wake kwa benchi la ufundi la timu hiyo.

Reha itakuwa na mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya timu kubwa ya Azam FC, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Jumapili saa 2.00 asubuhi.

Azam U-20 imekuwa na kiwango kizuri tokea ifanye usajili mkubwa hivi karibuni, ambapo mwezi uliopita ilifanya ziara ya wiki mbili kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikicheza jumla ya mechi 11, ikishinda sita, sare nne na kupoteza moja huku ikifunga jumla ya mabao 16 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane.

Mechi ilizoshinda, ilizichapa Makambako Combine (3-0), Polisi Njombe (4-1), Mbinga City (3-2), Mbinga Combine (2-1), Tunduru Combine (1-0) na Newala Combine (1-0), ilitoka sare na timu ya Daraja la Pili, Ihefu FC (0-0), Sudeco FC (0-0), Masasi Rangers (0-0) na Namungo FC (0-0), ambayo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza.