TIMU ya Azam Veteran inatarajia kushiriki michuano ya Urafiki Cup itakayofanyika kuanzia kesho Ijumaa hadi Oktoba 12 mwaka huu kwenye Viwanja vya Gymkhana, Posta, jijini Dar es Salaam.

Jumla ya timu nyingine sita zinatarajia kushiriki michuano hiyo itakayokuwa kwa mfumo wa ligi, ukiondoa Azam nyingine zinazoshiriki ni wenyeji Gymkhana Veteran, Mikocheni Veteran, Dar Veteran, Bin Slum Veteran na JMK Park Veteran.

Azam Veteran itafungua dimba kwa kuvaana na Mikocheni Veteran saa 1.30 usiku, mechi itakayotanguliwa na ile ya ufunguzi kati ya wenyeji Gymkhana watakaomenyana na Dar Veteran, zote zikiwa ni mechi za wiki ya kwanza.

Aidha Azam Veteran ambayo nahodha wake ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’, imekuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi kila wiki katika siku za Jumatatu, Jumatano na kucheza mechi Ijumaa ya kila wiki.

Baadhi ya wachezaji wengine wa kikosi hicho ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC, Nassor Idrissa ‘Father’, Meneja wa timu, Phillip Alando.