KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Transit Camp na Arusha United kwa ajili ya kujiweka sawa.

Benchi la ufundi la Azam FC limeamua kufanya hivyo ili kuwaweka kwenye ushindani wachezaji ambao hawajacheza mechi mbili za awali za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), ambayo imesimama.

Ligi hiyo imesimama kupisha mechi ya kufuzu Mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon kati ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na Uganda ‘The Cranes’ itakayofanyika jijini Kampala Septemba 8 mwaka huu.

Meneja wa timu hiyo, Phillip Alando, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa Azam FC itaanza kucheza dhidi ya Transit Camp mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru keshokutwa Jumamosi saa 3.00 asubuhi.

Alisema mara baada ya mchezo huo, watacheza dhidi ya Arusha United Jumanne ijayo utakofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 12.00 jioni.

“Transit Camp walituomba na walikuwa na tukio lao, na mwalimu ameona ni wasaa mzuri kwa wachezaji ambao hawajapata nafasi ya kucheza ili waweze kupata uzoefu au waweze kupata mechi za majaribio.

“Jumanne tutacheza na Arusha United hii ni timu kutoka Arusha ipo Ligi Daraja la Kwanza wapo katika ziara yao ukanda huu wa Pwani wakitoka kucheza na Namungo watapita hapa Dar es Salaam tutacheza nao Jumanne kwenye Uwanja wa Azam Complex,” alisema.

Aidha alisema mechi hizo mbili zitampa nafasi nzuri kocha kuwaona wachezaji ambao hawajapata nafasi ya kucheza mechi mbili za ligi.

Jumla ya wachezaji saba wa Azam FC, wameripoti timu mbalimbali za Taifa, nahodha Agrey Moris na msaidizi wake, Frank Domayo, Mudathir Yahya, David Mwantika na Yahya Zayd wakiwa kambini kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Wachezaji wengine wawili wa kigeni, beki wa kulia Nickolas Wadada akiwa timu ya Taifa ya Uganda, huku kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu, akitarajiwa kujiunga na Zimbabwe kesho Ijumaa.