KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itabakia nyumbani kwenye mchezo wake wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu huu ikicheza dhidi ya Ndanda keshokutwa Jumatatu saa 2.00 usiku.

Azam FC ilianza vema msimu mpya wa ligi kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City, yaliyofungwa na Joseph Mahundi na Danny Lyanga.

Wapinzani wao Ndanda nao wameanza kwa ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Ruvu Shooting, mchezo uliofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.

Kikosi cha Azam FC kitarejea leo Jumamosi jioni kuanza rasmi mazoezi kujiandaa na mchezo huo kikiwa chini ya Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm.

Wakati ikijiandaa kucheza na timu hiyo kutoka mkoani Mtwara, tunakuletea takwimu muhimu za timu hizo zilipokutana kwenye mashindano mbalimbali rasmi.

Mechi zilipokutana  

Azam FC iliyopanda rasmi Ligi Kuu mwaka 2008, imekutana na Ndanda mara tisa kwenye mechi za mashindano mbalimbali, ikikutana nayo mara nane Ligi Kuu na mara moja kwenye Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Safari hii itakuwa ikikutana nayo kwa mara ya 10, ambapo katika mara tisa walizokutana awali, Azam FC imeshinda mechi sita, sawa na asilimia 54, imetoka sare mara mbili huku Ndanda ikishinda miwili, yote ndani ya Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Katika mechi hizo tisa za awali walizocheza, jumla ya mabao 20 yamefungwa, Azam FC ikitupia 13 kwenye nyavu za wapinzani wao hao huku ikiruhusu mabao saba kutoka Ndanda.

Katika mechi pekee za ligi hiyo, wamekutana mara nane, matajiri hao wakishinda mara tano, sare moja na kupoteza mechi mbili.

Ndanda vs Azam Complex

Rekodi zinaikaba Ndanda ambayo ina rekodi mbaya kila inapocheza kwenye Uwanja wa Azam Complex, ambapo katika mechi zote za mashindano imekutana na Azam FC mara tano ndani ya simba hilo ikifanikiwa kuvuna sare moja tu na kuambulia vichapo mechi nne zilizobakia ikiwemo ile ya ASFC.

Mechi hiyo ambayo Azam FC ililazimishwa sare  ilikuwa ni msimu 2015/2016 ikiisha 2-2, mabingwa hao wakitangulia kwa mabao mawili yaliyofungwa na Didier Kavumbagu na Singano, huku Ndanda ikisawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Atupele Green (penati) na Ahmed Msumi.  

Ushindi wa kukumbukwa

Ni mara mbili tu, Azam FC imeweza kuibuka na ushindi mnono dhidi ya Ndanda, mara ya kwanza ikiwa kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) Aprili 5 mwaka jana ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Mabao ya Azam FC kwenye usiku huo yalifungwa na mshambuliaji aliyetimkia CD Tenerife ya Hispania, Shaaban Idd, aliyefunga mawili huku Ramadhan Singano ‘Messi’ akitupia jingine.

Ushindi wa pili wa kukumbukwa ulikuwa kwenye ligi msimu uliopita ukiwa ni mchezo wa raundi ya pili Februari 3, 2018, Azam FC ikipata tena ushindi wa 3-1, mabao yakiwekwa kimiani na Shaaban tena, Yahya Zayd na winga Enock Atta.

Msimu wa kukumbukwa   

Katika misimu yote minne waliyokutana, ni mara moja tu Azam FC imeweza kuvuna pointi sita kwenye mechi mbili za msimu wa ligi, ikifanya hivyo msimu uliopita (2017-2018).

Azam FC ilianzia ugenini kwa kuichapa Ndanda bao 1-0 kwenye mechi ya ufunguzi msimu uliopita, bao lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo kutoka Ghana, Yahaya Mohammed, kabla kuichapa 3-1 katika Uwanja wa Azam Complex.

Msimu mwingine ambao Azam FC ilipata pointi nyingi dhidi ya Ndanda, ni ule 2015-2016 ikifanikiwa kuvuna pointi nne, ikiichapa Ndanda ugenini bao 1-0 lililofungwa na beki wa kulia Shomari Kapombe, akimalizia kwa kichwa krosi safi ya Kipre Tchetche (wote wakiwa hawapo kikosini hivi sasa), huku kwenye mchezo wa raundi ya pili ikipata sare ya 2-2.

Mfungaji bora wa mechi hizo

Shaaban ndiye anashikilia rekodi ya Azam FC ya kufunga mabao mengi dhidi Ndanda, akiwa amefunga matatu akifuatiwa na Yahaya Mohammed na Ramadhan Singano, ambao kila mmoja amefunga mawili.