KOCHA Mkuu wa wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amefurahishwa na ushindi dhidi ya Mbeya City usiku wa kuamkia leo, huku akiwaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi zaidi kuelekea mechi zijazo.

Azam FC ilianza vema mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kwa kuifunga Mbeya City mabao 2-0 yaliyofungwa na winga Joseph Mahundi na mshambuliaji Danny Lyanga, ushindi uliowawezesha kukaa kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi tatu na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, Pluijm alisema kuwa mashabiki wa timu hiyo wanapaswa kuja kwa wingi zaidi ili kuwapa sapoti wachezaji wa timu hiyo.

“Nafikiri tulifanya mazoezi vizuri wiki hii kwa upande mwingine tungeweza kufunga bao la tatu na la nne katika hatua nyingine tulicheza dhidi ya mpinzani (Mbeya City) bora sana waliamini wanaweza kupata chochote kuanzia mwanzo wa mchezo hadi mwisho

“Walikuwa wagumu wakati wote, wanacheza kwa nguvu sana katika kuwania mipira, tulijiandaa kwa hilo na niliwaambia wachezaji wangu kabla kuwa kila mpinzani ataonyesha zaidi anapocheza dhidi ya Azam wakati mwingine dhidi ya Yanga au Simba wakitaka kuonyesha kwa wote kuwa wanaweza,” alisema.

Aidha alisema anafurahishwa na ushindi huo huku akikiri kuwa yangeweza kuwa mengine kama Mbeya City wangefunga penalti dakika ya 76 iliyokoswa na Eliud Ambokile, kufuatia kipa wa Azam FC, Razak Abalora, kumwangusha ndani ya eneo la hatari Chunga Said, aliyeunasa mpira ulioanzishwa vibaya na kipa huyo.

“Huwezi kujua kingetokea nini baada ya Mbeya City kufunga penalti ile, lakini naona mwanga wa mabadiliko na ndio maana nimekuwa nikiwaambia wachezaji wangu kuwa tunatakiwa kuendelea kupambana kila wiki dhidi ya wapinzani wagumu hasa tunatakiwa kushinda mechi za nyumbani,” alisema.

Hali ya kupambana

Akizungumza hali ya kupambana kwa wachezaji wake wote walioanza na walioingia kipindi cha pili, Pluijm alisema amefurahishwa na hilo akidai kuwa mashabiki wanamatarajio ya kuona kitu kama hicho wanapokuja uwanjani.

“Nashukuru kila mchezaji ameonyesha hiko kitu nimeshawaambia nina wachezaji 25 kikosini na wakati huu wachezaji wawili hawapo ambao ni majeruhi katika upande mwingine wote wanaweza kucheza na hakuna anayefikiria kama yupo chini au hana kiwango kila mmoja anaweza kucheza na hiko ndicho wameonyesha.

“Nina furaha sana kuna ari ya kujitoa kwenye timu na uwajibikaji mzuri kati ya vijana,” alisema kocha huyo aliyeinoa Singida United msimu uliopita, huku akionyesha sura yenye furaha.

Mechi na Ndanda  

Kuelekea mchezo wa pili wa ligi dhidi ya Ndanda utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Jumatatu ijayo saa 2.00 usiku, Pluijm alisema kuwa wanatakiwa kujiandaa vema kutokana na mchezo huo kuwa mgumu.

“Tutapumzika siku moja kesho (leo), tutakayotumia kwa ajili ya kuwarejesha vema wachezaji (recovery), Jumamosi jioni tutafanya mazoezi, Jumapili jioni tutafanya mazoezi na Jumatatu tunatakiwa kuwa tayari kwa mpambano mwingine.

“Angalia ukisema itakuwa mechi rahisi, mimi nitakuwa nimedanganya kwa sababu mechi zote zinatarajia kuwa ngumu nilieleza mwanzoni kwenye mahojiano haya, kila mmoja anataka kuonyesha kitu dhidi ya Azam, Simba na Yanga,” alisema.

Mholanzi huyo aliongeza kuwa: “Nafikiri kuna wachezaji wengi wanataka kucheza hapa haitakuwa uwezo wa kuonyesha wa mchezaji mmoja mmoja bali timu nzima kama unavyoona walivyopambana (Mbeya City) hadi dakika ya mwisho.”   

Wachezaji wa Azam FC waliokuwa majeruhi hadi sasa ni beki Yakubu Mohammed na mshambuliaji Donald Ngoma, ambaye anamalizia programu ya mwisho ya kujiweka fiti baada ya kukaa nje ya dimba kwa muda mrefu. Beki Daniel Amoah, naye anaendelea vema kuuguza majeraha yake ya goti yatakayomuweka nje ya dimba hadi Februari mwakani.

Kuangalia Mahojiano Yote, Fuata Link Hii ya Ukurasa Wetu Rasmi wa YouTube: https://youtu.be/t0_rJXaO-mw