USHINDI wa mabao 2-0 ilioupata Azam FC dhidi ya Mbeya City umeifanya kuanza vema msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) 2018-2019 baada ya kukaa kileleni kwenye msimamo.

Azam FC imekaa kileleni baada ya kujikusanyia pointi tatu na sawa na timu nyingine sita lakini ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga huku ikiwa haijafungwa bao lolote.

Timu nyingine sita zinazoifuatia zikiwa na pointi hizo ni Kagera Sugar, Stand United, Ndanda, Mbao, Simba na Yanga, ambazo nazo zimeshinda mechi za ufunguzi za ligi hiyo yenye timu 20 msimu huu.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, aliiongoza kwa mara ya kwanza timu hiyo kwenye mechi ya mashindano tokea aajiriwe msimu huu sambamba na Msaidizi wake, Juma Mwambusi, huku pia akiwaanzisha wachezaji wapya watatu kikosini beki wa kulia Mganda, Nickolas Wadada, kiungo Mudathir Yahya aliyerejea nyumbani pamoja na washambuliaji Tafadzwa Kutinyu na Danny Lyanga.

Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) mara mbili mfululizo wenye maskani yao Azam Complex, walianza kwa kasi ya chini mchezo huo lakini iliwasha moto wake kuanzia dakika ya 25.

Baada ya kurejea mchezoni kwa kasi kubwa ilifanikiwa kupata bao la uongozi dakika ya 32 lililofungwa kiustadi na winga Joseph Mahundi, aliyekuwa kwenye ubora mkubwa usiku huu ambaye alimalizia kwa shuti mpira wa kichwa aliodondoshewa na mshambuliaji mpya Lyanga.

Lyanga aliyekuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya mashindano tokea ajiunge na Azam FC msimu huu, alidondosha pande hilo kwa Mahundi baada ya kupigiwa krosi safi ya juu na Nahodha Msaidizi Frank Domayo, ‘Chumvi’.

Mahundi anafanikiwa kuandika rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Azam FC kufunga bao la kwanza la kufungua msimu wa ligi kwa timu hiyo, ambalo msimu uliopita lilifungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa matajiri hao, Yahaya Mohammed, wakati wakiilaza Ndanda bao 1-0.

Wakati watu wakidhani mpira ungeenda mapumziko kwa bao hilo, ubao wa matokeo uligeuka tena kwa bao la pili la Azam FC, lililofungwa kiufundi na Lyanga, akimalizia pasi ya mpenyezo ya kiungo Mudathir, iliyookolewa vibaya na nahodha wa Mbeya City, Erick Kyaruzi.

Kipindi cha pili Azam FC ilirejea tena kwa kasi na kukosa nafasi kadhaa za kuongeza mabao zilizopotezwa na mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu, Mahundi huku kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, aliyeingia dakika 10 za mwisho za mchezo huo akipiga mashuti mawili hatari langoni mwa Mbeya City.

Mbeya City walilazimika kucheza pungufu kwa dakika 23 za mwisho za mchezo huo, baada ya mchezaji wao Ramadhan Malima, kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya Kutinyu, aliyekuwa tayari amemtoka tayari kwa kuleta madhara langoni mwa Wanakomakumanya hao.

Dakika ya 76 kipa wa Azam FC, Razak Abalora, alifanya kazi ya ziada kuokoa mkwaju wa penalti uliopigwa na mshambuliaji, Eliud Ambokile na kuinyima Mbeya City nafasi ya kufunga.

Adhabu hiyo ya mkwaju wa penalti imetokana na kipa huyo kumwangusha ndani ya eneo la hatari Chunga Said, wakati akiwa kwenye harakati za kufuta makosa ya kuuanzisha vibaya mpira ulionaswa na mshambuliaji huyo.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika Ijumaa kabla ya kurejea mazoezini Jumamosi kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya Ndanda utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumatatu ijayo saa 2.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Joseph Mahundi, Frank Domayo/Sure Boy dk 80, Danny Lyanga, Tafadzwa Kutinyu/Yahya Zayd dk 80, Ramadhan Singano