WACHEZAJI watatu wa Azam FC wamejumuishwa kwenye kikosi kipya cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani dhidi ya Uganda Septemba 8 mwaka huu jijini Kampala, Uganda.

Stars ipo Kundi L sambamba na Capeverde, Lesotho na Uganda, hadi sasa ikiwa imecheza mchezo mmoja dhidi ya Lesotho na kutoka sare ya bao 1-1.

Wachezaji wa Azam FC walioitwa na Kocha Mkuu mpya wa Stars, Emmanuel Amunike, ni nahodha Agrey Moris, kiungo Mudathir Yahya na mshambuliaji Yahya Zayd.

Kikosi hicho cha wachezaji 25 kinaundwa na makipa, Aishi Manula (Simba SC), Mohammed Abdulrahman (JKU), Benno Kakolanya (Yanga SC), mabeki ni Shomari Kapombe (Simba SC), Hassan Kessy (Nkana FC, Zambia), Gardiel Michael (Yanga SC), Abdi Banda (Baroka FC, Afrika Kusini), Kelvin Yondan (Yanga SC), Agrey Moris (Azam FC) na Andrew Vincent (Yanga SC).

Viungo ni Himid Mao (Petrojet FC, Misri), Mudathir Yahya (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Erasto Nyoni (Simba SC), Simon Msuva (Difaa Hassan El-Jadida, Morocco), Shiza Kichuya (Simba SC), Farid Mussa (CD Tenerife, Hispania), Feisal Salum (Yanga SC) na Hassan Dilunga (Simba SC).

Washambuliaji ni Rashid Mandawa (BDF XI, Botswana), Yahya Zayd (Azam FC), Shaaban Idd Chilunda (CD Tenerife, Hispania), John Bocco (Simba SC), Emmanuel Ulimwengu (El Hilal, Sudan) na Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji).

Uganda, Zimbabwe wamo

Wakati huo huo, wachezaji wengine wa kimataifa wa Azam FC, beki wa kulia Nickolas Wadada, ameitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ itakayocheza na Stars, sambamba na kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu, aliyeitwa timu ya Taifa ya Zimbabwe ‘The Warriors’, itakayokuwa ikijiandaa kucheza na Congo Brazzaville katika kufuzu fainali hizo zitakazofanyika nchini Cameroon.