ZIKIWA zimebakia siku tano kabla ya kufunguliwa kwa pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), uongozi wa Azam FC umekutana na mashabiki wa timu hiyo kupanga mikakati ya mafanikio.

Azam FC itafungua pazia hilo Agosti 23 kwa kukipiga na Mbeya City, mchezo unaotarajia kufanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam saa 1.00 usiku.

Kwa upande wa uongozi wa Azam FC, uliwakilishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin ‘Popat’ na Meneja wa timu, Phillip Alando, ambao walikuwa wakijibu maswali mbalimbali ya mamia ya mashabiki waliohudhuria.

Mbali na kujibu maswali pia walishiriki kwa pamoja kupanga mikakati kuelekea msimu ujao ya namna ya kusapoti wachezaji kwa mechi za nyumbani na ugenini.

Kikao hicho kilichochukua saa nne kilihitimishwa kwa chakula cha pamoja na picha za ukumbusho kwa wote waliohudhuria huku mashabiki wakielezea furaha zao kwa viongozi kutokana na ukaribu waliouonyesha.

Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Kombe la Kagame na Mapinduzi, wamejipanga vilivyo kufanya vema msimu huu wakifanya usajili mzuri pamoja na kuchukua makocha wazoefu wa soka la Tanzania, Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi.