KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo asubuhi imeanza rasmi maandalizi kuelekea mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Mbeya City.

Azam FC imeanza kujinoa zikiwa zimesalia siku tano tu kuelekea mchezo huo, unaotarajia kufanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Alhamisi ijayo saa 1.00 usiku.

Wachezaji wa timu hiyo walifanya mazoezi ya kawaida ya kujenga ufiti kabla ya mwishoni kuhamia kwenye programu ya kucheza mechi fupi ya nusu uwanja ya mtoano, wakigawanywa katika makundi matatu.

Katika kujiandaa vema na mchezo huo, kikosi hicho kitaendelea na mazoezi mengine jioni ya leo, kesho Jumapili itafanya mengine na wiki ijayo kumalizia programu ya mwisho kabla ya kukwaana na wapinzani wao Alhamisi.

Nyota wawili waliopata majeraha kwenye kambi ya nchini Uganda, mshambuliaji Danny Lyanga na winga Idd Kipagwile, wameanza rasmi mazoezi ya kawaida na wenzao leo huku waliobakia winga Joseph Kimwaga na mshambuliaji Donald Ngoma, wakiendelea na mazoezi mepesi ya kujiweka sawa.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Juma Mwambusi, ameshaweka wazi kuwa kambi ya Uganda imewasaidia kuwaweka pamoja na wachezaji na kilichobakia hivi sasa ni kurekesbisha mapungufu kadhaa kabla ya kuingia kwenye ligi wiki ijayo.