WACHEZAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, wameeleza kuwa kambi waliyomaliza nchini Uganda itawapa mwanga mzuri kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).

Azam FC iliyokuwa imeweka kambi ya wiki mbili nchini humo, tayari imemaliza kambi hiyo ikiwa imecheza jumla ya mechi tatu, ikitoka sare mbili dhidi ya URA (0-0), Express (1-1) na kufungwa na KCCA (4-2).

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kwa niaba ya wachezaji wenzake, Nahodha Mkuu Agrey Moris, ameelezea kufurahishwa na kambi hiyo huku akidai kuwa imewaongezea hali ya kujiamini zaidi.

“Hii ndivyo inavyotakiwa kama timu kipindi cha maandalizi itoke kwenda nje kutafuta mechi ili kujiandaa na kuipima timu na kuijua ipoje, wachezaji wote wamefurahia kambi wapo katika morali ya hali ya juu hii inaashiria ishara nzuri kwa timu kama yetu.

“Mnapotoka kama hivi halafu wachezaji wanafurahia kitu hiki kinaonyesha mwanga mzuri katika ligi mnapoelekea, mashabiki waendelee kuisapoti timu yao kwa sababu tunawategemea sana kwa sapoti yao, ila wasichoke tu waje kuisapoti timu na sisi tutawapa kile wanachohitaji,” alisema.

Naye Kocha Msaidizi wa Azam FC, Juma Mwambusi, alisifia kambi kiujumla na kudai kuwa wao kama benchi la ufundi wameshajua mapungufu ya timu ambayo watayafanyia kazi kabla ya ligi hiyo kuanza Agosti 22 mwaka huu.

“Kikosi kinaonyesha mwanga ukizingatia wachezaji wengi wapo Azam kwa muda mrefu na wachezaji wapya wapo wachache ambao bado ndio wanaingia kwenye mfumo nadhani na mwalimu ni mpya

“Kwa hiyo kila kitu kinaenda kwa kutegemeana wachezaji, mwalimu na vilevile muda tuliokuwa nao na mbinu zinakwenda vizuri na wachezaji wanaonekana wanaonyesha mwanga kwamba wanaweza kutusaidia kufanya vizuri,” alisema Mwamusi alipozungumzia maendeleo ya kikosi hicho.

Mara baada ya kumaliza ziara hiyo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kesho Alhamisi saa 8 mchana tayari kumalizia maandalizi ya mwisho kabla ya kufungua pazia la ligi Agosti 23 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.