KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Hans Van Der Pluijm, amesema kuwa hatua kwa hatua kikosi chake kitakuwa vizuri kuelekea msimu ujao 2018-2019.

Azam FC inaelekea kuhitimisha maandalizi ya msimu ujao ikiwa nchini Uganda kwa kambi ya wiki mbili tokea Julai 30, ikitarajia kurejea jijini Dar es Salaam Alhamisi hii mchana.

Ikiwa kwenye kambi hiyo, mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Kombe la Kagame na Mapinduzi, wamecheza mechi tatu za kujipima nguvu ikitoka sare mbili dhidi ya URA (0-0), Express (1-1) na kupoteza mmoja KCCA (4-2).

Pluijm ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa kwa sasa anachoangalia ni kuandaa ufiti na ari ya kupambana kwa wachezaji wake, likiwa ndio jambo la msingi kwenye kipindi cha maandaalizi ya msimu.

“Kwangu mimi ari ya kupambana ndio jambo la msingi unalotakiwa kuwa nalo kwanza kwenye timu, kama ukiwa na ari ya kupambana na kimwili uko fiti unaweza kushinda kwa mpinzani yoyote na hilo ndilo unapaswa kufanya,” alisema.

Akizungumzia mechi tatu walizocheza, alisema: “Narudia kusema tena kwa sasa matokeo si kitu, jambo la muhimu ni kuhakikisha timu inakuwa fiti, bado tuna wiki mbili za kufanya kazi ili kuweka mambo sawa, ukiangalia kuna utofauti tulivyocheza dhidi ya KCCA na Express, naamini hatua kwa hatua tutakuwa vizuri zaidi.”   

Ikiwa inakamilisha kambi yake nchini hapa, Azam FC itaendelea na programu ya mazoezi ya kawaida kila siku na kurejea Dar es Salaam kumalizia maandalizi ya mwisho kabisa, kabla ya kuivaa Mbeya City kwenye mechi yake ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex Agosti 23 mwaka huu saa 1.00 usiku.