MSHAMBULIAJI wa zamani wa Azam FC, Shaaban Idd, ametua rasmi nchini Hispania kwenye klabu yake mpya ya CD Tenerife aliyojiunga nayo kwa mkataba wa miaka miwili.

Chilunda, 20, aliyekuwa akisubiria kukamilika kwa taratibu za kutafuta kibali cha kufanya kazi nchini Hispania, alitarajiwa kutua nchini humo leo saa 4.55 asubuhi kwa saa za Tanzania kabla ya kufanyiwa vipimo saa 9.00 alasiri.

Nyota huyo anakuwa mchezaji wa pili wa Azam FC kujiunga na timu hiyo inayopambana kupanda Ligi Kuu Hispania (La Liga), wa kwanza akiwa winga Farid Mussa, ambaye amejumuishwa katika kikosi cha timu ya kwanza ya Tenerife inayojiandaa na msimu mpya.

Mfungaji huyo bora wa Azam FC msimu uliopita akifunga jumla ya mabao 11, anakwenda huko akitoka kuwa mfungaji bora wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) akitupia mabao nane kwenye mechi tano.

Azam FC tunachukua fursa hii kumtakia kila la kheri kwenye maisha yake mapya ndani ya timu hiyo, akafanikiwe zaidi na kuzidi kusonga mbele ndani ya muda mfupi ujao.