WAKATI zikiwa zimesalia siku 15 kabla ya pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) msimu mpya 2018/2019 kufunguliwa, habari njema ni kuwa mshambuliaji mpya wa Azam FC, Donald Ngoma, yuko kwenye hatua za mwisho kurejea dimbani.

Nyota huyo ambaye tayari ameanza mazoezi mepesi ya kujiweka sawa, kwa sasa anafanya mazoezi makali ya gym kwa muda wa dakika 90 kila siku kambini nchini Uganda, akitafuta ufiti wa viungo kwa mujibu wa programu aliyopewa.

Programu hiyo ataendelea nayo hadi atakaporuhusiwa kurejea dimbani kucheza na wenzake wiki chache zijazo.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Ngoma alisema kuwa kwa sasa hasikii maumivu yoyote katika goti lake la mguu wa kulia huku akidai anachozingatia hivi sasa ni kufanya mazoezi ya kurejesha ufiti.

“Kitu cha kwanza nataka kumshukuru sana Mungu kwa sababu naendelea vizuri na sasa hivi sisikii maumivu na natafuta ufiti na najua nikiendelea kama hivi wiki mbili hadi tatu naweza kurejea uwanjani,” alisema.

Ngoma ameizungumzia programu anayopewa hadi sasa na kukiri kuwa imemsaidia sana kiasi kwamba hasikii maumivu yoyote kwenye goti lake na kudai imebakia kazi ya kutafuta ufiti tu.

Msimu ujao

Straika huyo hatari kutoka nchini Zimbabwe, ameweka wazi kuwa kwa sasa kitu muhimu kwake ni kutengeneza ufiti huku akidokeza jambo la pili kubwa kwa msimu ujao ni kutwaa makombe akjwa na Azam FC.

“Sijacheza mpira muda mrefu sana hivyo kitu cha kwanza ni kutafuta ufiti cha pili ni kuchukua ubingwa, kwa sababu ndio kitu kilichofanya nikasajiliwa hapa Azam FC hivyo tunataka ubingwa,” alisema.

Azam FC kiujumla

Nyota huyo aliyewahi kuzichezea Platinums ya Zimbabwe na Yanga, aliisifia Azam FC akidai ni klabu tofauti sana na nyingine ikiongozwa kiuweledi.

“Kitu cha muhimu sana ni kucheza vizuri, ukicheza vizuri na maisha yako yanaendelea vizuri, nafikiri ni changamoto mpya kwangu, tunatakiwa kushinda mechi na pia kutwaa ubingwa wa ligi, hili ni jambo la muhimu sana.

“Kuchukua ubingwa ni jambo la muhimu sana kwa mashabiki wa timu yangu ya Azam hivyo kwa sasa naangalia mbele kuwa tutashinda ubingwa,” alisema.

Nipo nyumbani kabisa  

Ngoma ambaye anasifika kwa kasi yake kubwa ya kushambulia, kufunga na kuwaweka kwenye wakati mgumu mabeki wa timu pinzani, alizungumzia pia ushirikiano anaopewa na wachezaji wenzake na kudai kuwa anajisikia kama yupo nyumbani.

“Hapa najisikia kama nipo nyumbani kwa sababu nimecheza muda mrefu sana hapa Tanzania miaka mitatu, nipo kama nyumbani wachezaji wengine nawajua na wenyewe wananijua kwa hiyo najisikia kama nipo nyumbani na tunasaidiana, tunaongea vizuri, tunbadilishana habari.

“Kwa hiyo sijisikii kama mgeni nafanya kama nipo nyumbani ni jina la timu tu nimebadilisha lakini nipo nyumbani,” alisema.

Kugombea namba

Katika hatua nyingine amekiri kuwa na ushindani wa namba kwenye kikosi cha Azam FC, akidai kuwa jambo hilo linasababishwa na timu hiyo kuwa na wachezaji wazuri sana.

“Unajua Azam ni timu nzuri sana kuna wachezaji wazuri sana na kuna ushindani mkubwa sana sio ukifika hapa unaingia kikosi cha kwanza lazima utapambana kuingia kwa sababu kuna wachezaji wazuri sana wana uwajibikaji mzuri sana.

“Nafikiri kwangu ndio kitu kitakuwa kigumu sana kuingia kwenye kikosi sio nitaingia kirahisi, nitafanya kazi mpaka nipate namba niingie kwenye kikosi cha kwanza,” alisema.

Msaada wa Mungu

Aidha Ngoma amekiri kuwa ni jambo gumu duniani timu kusajili mchezaji aliye majeruhi, hivyo anafikiria kwake yeye imetokana na msaada wa Mungu huku akiupongeza uongozi wa Azam FC.

“Sio rahisi kufanyika kwa kitu ambacho wamenifanyia mimi kumsajili mtu majeruhi, kwa sasa wanaamini kuna kitu nitaongeza kwenye timu hivyo najisikia mwenye furaha sana nafikiri hii inaonyesha uweledi wa timu na nafikiri wanatarajia kitu kikubwa kutoka kwangu ninachotarajia kukifanya.

“Kama Mungu atajalia nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu ili kushinda na kufanya vizuri,” alisema.

Mpira wa Tanzania

Akiwa amecheza Tanzania kwa kipindi cha miaka mitatu tokea alipojiunga na Yanga mwaka 2015, ameelezea utofauti wa soka la Tanzania na Zimbabwe, akidai soka la hapa linahitaji umakini wa hali ya juu.

“Linhitajia umakini wa hali ya juu kwa sababu kuna vitu vingi vinatokea, nimecheza timu kama Yanga unahitaji kuwa nguvu ya akili, pia Tanzania presha iko juu ambayo inakuhamasisha na kukufanya ufanye vizuri na ligi pia ni ya ushindani sana na ya nguvu inayokutaka uwe imara, pia kuna vipaji vingi sana.

“Ni ligi nzuri ukilinganisha na ile ya Zimbabwe kitu tofauti ni unatakiwa kuwa na nguvu sana, utumie nguvu sana na wakati mwingine unakutana na timu iliyo chini kwa ligi lakini itakupa ugumu sana kuifunga, ligi ya Zimbabwe wanatumia vipaji sana na kuna vipaji vingi sana, hapa Tanzania kuna kipaji na lazima utumie nguvu pia,” alisema.

Kuungana na Pluijm

Ngoma amefurahi sana kuungana tena na kocha wake wa zamani, Hans Van Der Pluijm, aliyewahi kumfundisha akiwa Yanga, na kudai ni kocha anayemjua vilivyo.

“Mwalimu (Pluijm) ananielewa sana, anajua tabia yangu na mimi najua kitu anachotaka, anataka mchezaji anayefanya kazi kwa bidii na mimi kwangu siwezi kuficha hicho ananiona kama mtoto wake, ananisaidia kama nikipotea, ananiambia ukweli.

“Kuna vitu huwa anavihitaji kutoka kwangu na najua anachotaka, anajua ninachoweza kufanya, namwelewa sana na yeye ananielewa, kwangu mimi itanipunguzia presha, kwa hiyo sitakuwa kwenye presha, najua anavyotaka mimi kufanya kazi na najua anachotarajia kutoka kwangu kwa hiyo nafikiri mimi ni mtu mwenye bahati,” alisema huku akitabasamu.

Nje ya uwanja

“Tabia yangu mimi huwa ni ile ile, napenda sana kukimbia wakati mwingine watu hunifikiria sana na kudhani kuwa mimi ni sipendi utani, siko hivyo napenda kutaniana na watu na kukaa ndani ya nyumba kuangalia luninga,” alisema.

Mashabiki wa Azam FC  

Ngoma anayemudu kuongea lugha ya Swahili kwa kiasi kikubwa, amewaachia neno mashabiki wa Azam FC akiwaambia kuwa furaha pekee watakayowaacha nayo ni kuwapa ubingwa.

“Kitu kinachoweza kufurahisha mashabiki wa Azam ni kuchukua ubingwa kwa sababu ndio kitu kilichotunileta hapa Azam, tunataka ubingwa nafikiri tuna timu nzuri sana, tukipambana tunachukua ubingwa na mashabiki watafurahi, viongozi watafurahi na sisi tutafurahi pamoja,” alimalizia Ngoma.

Kwa sasa kikosi cha Azam FC kipo kambini nchini Uganda kwa maandalizi ya msimu ujao, kikitarajia kurejea Tanzania Agosti 16 mwaka huu tayari kufungua pazia la ligi Agosti 23 kwa kucheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi saa 1.00 usiku.

N.B: Usikose kuangalia mahajiano yake kamili ya video hapo baadaye leo Jumanne kwenye kipindi cha Azam FC TV kinachoruka kupitia Kingamuzi cha Azam TV; kikianza kuruka katika Chaneli ya Azam Sports HD (saa 1.00 usiku) na Azam Sports 2 (saa 1.30 usiku). Vilevile utaipata kupitia Chaneli ya YouTube ya Azam FC ‘Azam Football Club’.