KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Jumatano itacheza mechi yake ya pili ya kujipima nguvu, ikikipiga dhidi ya moja ya timu matajiri nchini Uganda, Wakiso Giants, utakaofanyika Uwanja wa KCCA saa 8.00 mchana.

Azam FC ipo kambini nchini Uganda ikijiandaa na msimu ujao, ambapo mechi hiyo itakuwa ya pili baada ya awali Ijumaa iliyopita kukipiga na URA, mchezo uliomalizika kwa suluhu.

Wakiso inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Uganda, imechukuliwa na moja ya wafanyabiashara nchini humo na kusajili nyota kadhaa kama vile viungo Isaac Ntege, Hassan Wasswa, winga Steven Bengo, James Kasibante, Feni Ali, washambuliaji Karim Ndugwa, Ivan Kiweewa,  lengo likiwa ni kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa CECAFA Kagame Cup na Mapinduzi Cup, wapo kwenye maandalizi makali chini ya makocha wapya, Hans Van Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi huku ikiwa imefanya usajili mzuri kwa ajili ya kutwaa mataji msimu ujao.

Wachezaji waliosajiliwa ni mabeki Nicholas Wadada (Vipers), Hassan Mwasapili (Mbeya City), viungo Mudathir Yahya aliyerejea akitokea kwa mkopo Singida United, Tafadzwa Kutinyu (Singida United), washambuliaji Donald Ngoma (Yanga), Daniel Lyanga (Singida United) na Ditram Nchimbi (Njombe Mji).

Mara baada ya mechi hiyo, Azam FC inatarajia kumalizia zaira kwa mechi nyingine mbili dhidi ya washindi wa pili wa Ligi Kuu Uganda, KCCA Ijumaa hii (Agosti 10) kabla ya kukipiga na mabingwa wa zamani wa nchi hiyo, Express FC Agosti 12, mwaka huu.