NYOTA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Enock Atta, ameiongoza timu ya Taifa ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 (Ghana U-20) kuichapa Benin mabao 3-1 kwenye mchezo wa raundi ya tatu kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo mwakani (AFCON U-20).

Mchezo huo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Cape Coast nchini Ghana jana, ilishuhudiwa winga huyo wa Azam FC akianza kwenye kikosi cha kwanza akicheza dakika 88 za mchezo na kupika bao la pili la Ghana dakika ya 72 kufuatia kona aliyochonga kabla ya nahodha wa timu hiyo, Issahaku Konda, kuiunganisha kwa kichwa.

Kama si juhudi za kipa wa Benin, Katchon Abiola, huenda Atta aliyekabidhiwa jezi namba 10 anayotumia akiwa Azam FC, angeiweka mbele Ghana dakika 10 za mwanzo za kipindi cha pili lakini mchomo wake uliokolewa na kipa huyo na kuinyima nafasi muhimu Black Satellites.

Mabao mawili mengine ya Ghana U-20 yaliyohitimisha ushindi huo yalifungwa na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Richard Donsu, anayechezea WAFA ya nchini mwao huo.

Ghana ambayo imekaribia kufuzu kwa fainali hizo, inatarajia kucheza mchezo wa pili wa marudiano unatarajia kufanyika wiki ijayo nchini Benin.