KOCHA Mkuu wa Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Hans Van Der Pluijm, ameelezea kufurahishwa na namna vijana wake walivyoweza kupambana kwa nguvu dhidi ya URA.

Mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki wa maandalizi ya msimu ujao, ulifanyika Uwanja wa Taifa wa Mandela (zamani Namboole) na kushuhudiwa ukiisha kwa suluhu.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Pluijm alisema kuwa haukuwa mchezo rahisi huku akikiri timu yake kutotengeneza nafasi za wazi za kufunga mabao katika kila kipindi.

“La kwanza haukuwa mchezo rahisi walicheza mchezo wa kutumia nguvu, ilitubidi kuachia mipira kwa haraka, mashambulizi yetu kufanya kwa haraka, lakini yote haya baada ya mazoezi makali ya jana, sijafurahishwa na baadhi ya vitu walivyofanya kwenye mchezo wa leo.

“Uwanja haukuwa mrahisi ilikuwa ni ngumu kucheza ‘tachi’ moja (one touch), kwa upande mwingine hatukutengeneza nafasi kipindi cha kwanza, tulitengeneza moja tu, kipindi cha pili hatukutengeneza nafasi za wazi, nafasi moja tu ya mpira wa adhabu ndogo aliopiga Frank (Domayo),” alisema.

Kocha huyo raia wa Uholanzi aliyewahi kuzinoa Berekum Chelsea, Ashanti Gold, Yanga, Singida United, alisema kuwa amepanga kutumia wiki chache zilizobakia kurekebisha makossa yaliyotokea ili kuhakikisha anapika kikosi cha ushindani kinachocheza staili ya kushambulia.

“Tuna wiki chache za kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza lakini nimependa namna walivyojituma na kucheza kwa nguvu kukabiliana na mpinzani,” alisema.

Mbali na mchezo huo wa kwanza wa kirafiki, Azam FC iliyotwaa taji la CECAFA Kagame Cup na Mapinduzi Cup mara mbili mfululizo kila moja, inatarajia kucheza mechi nyingine tatu za kirafiki.