MABINGWA wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, wameanza kwa sare mechi ya kwanza ya kirafiki ya maandalizi ya msimu ujao baada ya kutoka suluhu na URA, mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa wa Mandela (zamani Namboole) jijini Kampala, Uganda.

Azam FC ipo kwenye kambi ya wiki mbili nchini humo, ziara itakayoambatana na mechi nne za kirafiki, ili kujiweka sawa na msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine unaoanza wiki chache zijazo.

Wachezaji wapya wa Azam FC, beki wa kushoto Hassan Mwasapili, kiungo Tafadzwa Kutinyu na mshambuliaji Danny Lyanga, walianza kuichezea kwa mara ya kwanza timu hiyo tokea wasajiliwe kwenye usajili mkubwa uliofungwa hivi karibuni.

Mechi hiyo ilianza kwa kasi kila timu ikilishambulia lango la mwenzie, lakini Azam FC ilionekana kufika sana langoni mwa URA ikitengeneza nafasi mbili dakika za mwanzoni.

Dakika ya 18 Lyanga, alijaribu kupiga shuti la mbali akipokea pasi la Kutinyu, lakini mpira ulikatika na kutoka nje.

Nahodha msaidizi wa Azam FC, Frank Domayo, aliichachafya safu ya ulinzi ya URA dakika ya 30 na kupiga shuti zuri nje ya eneo la 18 lakini kipa alionyesha umahiri baada ya kuupangua mpira na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Kuelekea dakika 15 za mwisho za kipindi cha kwanza mpira ulionekana kwenda sawa kwa pande zote mbili na kupelekea timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazijafungana.

Kipindi cha pili Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm, alifanya mabadiliko ya kiufundi akimtoa winga Idd Kipagwile na kumuingiza beki wa kushoto Hassan Mwasapili, akipewa majukumu ya winga wa kushoto huku Ramdhan Singano ‘Messi’, akihamishiwa winga ya kulia.

Mabadiliko hayo yaliongeza kasi, Azam FC ikifanya mashambulizi mfululizo langoni mwa URA lakini safu ya ulinzi ilisimama imara kuokoa hatari zote.

Dakika ya 49 Domayo alikaribia kuiandikia bao la uongozi Azam FC baada ya kupiga mpira mzuri wa faulo uliopanguliwa na kipa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Licha ya Azam FC kufanya mabadiliko mengine kadhaa ya kuingia mshambuliaji Mbaraka Yusuph na viungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Salmin Hoza, bado mpira huo ulimalizika kwa timu zote kutofungana.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitapumzika kesho Jumamosi kabla ya Jumapili kufanya tena mazoezi huku ikiwa imebakiza mechi nyingine tatu za kirafiki wakiwa kwenye kambi hiyo.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, David Mwantika, Mudathir Yahya/Sure Boy dk 75, Idd Kipagwile/Mwasapili dk 46, Frank Domayo (C), Danny Lyanga/Mbaraka dk 54, Tafadzwa Kutinyu/Hoza dk 83, Ramadhan Singano