KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimewasili salama nchini Uganda muda mchache uliopita kwa ajili ya kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na msimu ujao 2018-2019.

Msafara wa Azam FC uliiondoka jijini Dar es Salaama leo saa 1 asubuhi na ndege ya Shirika la Precision Airways ukipitia Kilimanjaro kabla ya kuunganisha Uganda, umesheheni wachezaji wote waliosajiliwa kwa msimu ujao isipokuwa nyota watatu Yakubu Mohammed, Enock Atta na Yahya Zayd.

Wakati beki Yakubu, akiuguza majeraha nyuma ya kifundo cha mguu wa kulia, winga Atta yupo timu ya Taifa ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 (Ghana U-17) huku Zayd akiwa kwenye majaribio ya kujiunga ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa programu ya benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi kikosi hicho kitafanya mazoezi ya kwanza jioni hii.

Azam FC ikiwa hapa nchini Uganda imefikia kwenye Hoteli ya Top Five, iliyopo Ntinda, jijini Kampala, ambapo inatarajia kucheza mechi nne hadi tano za kirafiki na timu za Vipers, KCCA, URA, Onduparaka na Express.