KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuondoka nchini kesho Jumatatu saa 1 asubuhi, kuelekea Uganda kuweka kambi ya wiki mbili kwa ajili ya kunoa makali ya msimu ujao 2018-2019.

Msafara wa Azam FC utakuwa na wachezaji wote waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao, isipokuwa beki Yakubu Mohammed, ambaye anauguza majeraha nyuma ya kifundo cha mguu wa kulia, winga Enock Atta aliyeko timu ya Taifa ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 (Ghana U-17) na Yahya Zayd aliyeenda kwenye majaribio ya kujiunga ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini.

Meneja wa timu hiyo, Phillip Alando, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa wamekamilisha taratibu zote za safari hiyo huku akieleza kuwa wanaamini ziara hiyo itasaidia kuwaunganisha vema wachezaji kuelekea msimu ujao.

“Matarajio ni wachezaji kufanya mazoezi ya pamoja kwa ajili ya kuiunganisha timu, kama mnavyoona kumekuwa na wachezaji wapya walioingia kwenye timu na makocha ni wapya, hivyo watatumia ziara hiyo kukipika vema kikosi kwa ajili ya kuleta ushindani msimu ujao,” alisema.

Kikosi hicho kikiwa nchini humo, kinatarajia kucheza mechi nne hadi tano za kirafiki na timu za huko, ambazo ni dhidi ya Mabingwa wa Uganda, Vipers, KCCA, URA, Onduparaka na timu kongwe ya Express.

Mara baada ya mechi hizo, mabingwa hao mara mbili mfululizo wa michuano ya CECAFA Kagame Cup na Kombe la Mapinduzi, watarejea jijini Dar es Salaam Agosti 16 mwaka huu kwa maandalizi ya mwisho ya Ligi Kuu inayotarajia kuanza kutimua vumbi kuanzia Agosti 22 huku Azam FC ikifungua dimba na Mbeya City Agosti 23 kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.  

Kocha Mkuu mpya Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi, wamefanya usajili wa wachezaji saba wapya ambao ni mabeki Nickolas Wadada, Hassan Mwasapili, viungo Tafadzwa Kutinyu, Mudathir Yahya alirejea kutoka kwa mkopo akitokea Singida United na washambuliaji Ditram Nchimbi, Donald Ngoma na Daniel Lyanga.

Ukiacha usajili huo, pia wachezaji wanne wametolewa kwa mkopo ambao ni kipa Metacha Mnata (Tanzania Prisons), mabeki Swaleh Abdallah (Singida United), Hamimu Karim (Mbao FC), Abbas Kapombe (Reha FC), Godfrey Elias (Polisi Tanzania), viungo Masoud Abdallah, Braison Raphael (wote KMC), Ismail Gambo (African Lyon).