IMETHIBITIKA kuwa mshambuliaji mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Donald Ngoma, atarejea dimbani Agosti 11 mwaka huu tayari kuanza kuitumikia timu hiyo kwa mechi za ushindani.

Baada ya kufanyiwa vipimo katika Hospitali ya Vincent Pallotti jijini Cape Town, Afrika Kusini katikati ya wiki hii, imebainika kuwa Ngoma amekutwa na tatizo la kuchanika mtulinga wa mbele wa goti la mguu wa kulia (Anterior Cruciate Ligament).

Daktari Mkuu wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa, aliyeongozana na Ngoma jijini humo, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa baada ya uchunguzi madaktari hao waliangalia mtulinga huo (ligament) na kubaini kuwa umeanza kupona, ambapo ataweza kurejea kwenye ushindani baada ya wiki tisa kupita kutoka sasa.

“Sasa matibabu yake ni nini, kwanza ni bahati yake kuwa yeye hatofanyiwa upasuaji atatakiwa kufanya mazoezi ya kawaida yasiyohusisha kulipa tabu goti lake (yatakayolishtua) kwa namna yoyote ile, katika wiki tatu hizi za kwanza kuanzia akiwa kwao Zimbabwe atatakiwa kufanya mazoezi madogo madogo.

“Atakaporudi hapa baada ya wiki tatu kupita kuanzia sasa, Ngoma atakuwa Chamazi (Azam Complex) na atakuwa akienda kwenye kliniki ya London Health Centre ataendelea na ile programu na kuanza kukimbia kwa kasi na ataruhusiwa kurejea uwanjani kwa mechi za ushindani kuanzia Agosti 11 mwaka huu,” alisema Mwankemwa kwa msisitizo.

Awazungumzia Yakubu, Amoah

Akiwazungumzia majeruhi wengine wa Azam FC, Mwankemwa alisema kuwa beki Yakubu Mohammed, aliyevunjika mguu na kukosa sehemu kubwa ya mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ameruhusiwa kuanza mazoezi tokea Juni Mosi mwaka huu.

Alisema beki mwingine Daniel Amoah, aliyefanyiwa upasuaji wa goti nchini Afrika Kusini atarejea dimbani baaada ya miezi tisa kupita tokea siku aliyoumia Februari mwaka huu, akimaanisha kuwa atarejea Oktoba mwaka huu.

“Mchezaji mwingine ni kijana wetu Stanslaus Ladislaus tuliyempelekea kwa mkopo African Lyon, tulimfanyia uchunguzi katika Hospitali ya Hi Tech naye amekutwa na tatizo la kuchanika mtulinga wa kati kwenye goti lake la mguu wa kulia na tunafanya taratibu hivi sasa za kumpeleka Afrika Kusini,” alisema.

Ngoma ni usajili mpya wa Azam FC kwa ajili ya msimu ujao na sasa ni wazi atakuwa fiti kucheza mechi za msimu ujao wa ligi akiwa na sura nyingine mpya, kama kiungo Tafadzwa Kutinyu, ambaye usajili wake umeshakamilika akitokea Singida United aliyoichezea msimu uliopita.  

KUANGALIA HABARI KAMILI; Bofya Linki hii <<<<  https://youtu.be/9m8zszi-Xh0 >>>>