TIMU ya vijana ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam U-20, imefungua pazia la michuano ya Ligi ya Vijana (U-20 Uhai Cup 2018) kwa kutoka suluhu dhidi ya Mtibwa Sugar leo mchana.

Michuano hiyo inafanyika kwenye viwanja vya Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), ambapo timu zote za vijana za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) zinashiriki zikiwa zimegawanywa katika makundi manne yenye timu nne kila moja, Azam U-20 ikiwa Kundi C.

Katika mchezo huo wa kwanza, timu zote zilijitahidi kucehza mpira lakini kwa kiasi kikubwa ugumu wa uwanja ulionekana kuondoa ladha ya mpira.

Hiyo ni sare ya pili kwa timu hizo ndani ya dakika 90, kwani kwenye mashindano yaliyopita Azam U-20 ilitinga fainali kwa kuchapa Mtibwa Sugar kwa mikwaju ya penalti 4-2 kufuatia dakika 120 kumalizika kwa suluhu.

Mchezo mwingine wa kundi hilo uliofuata kati ya Majimaji na Mwadui nao ulimalizika kwa suluhu, jambo ambalo linaweka uhuru wa timu zitakazofanya vizuri kwatika mechi mbili za mwisho za makundi kuweza kusonga mbele kwa hatua ya robo fainali.

Aidha mechi nyingine za Kundi A, Yanga imetoka suluhu na Ruvu Shooting huku Mbao ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City huku ikishuhudiwa kipa wao Metacha Mnata, aliyepo kwa mkopo akitokea Azam akiibuka shujaa baada ya kuokoa michomo mingi ya nguvu.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam U-20 kitapumzika kabla ya kushuka tena dimbani keshokutwa Jumatatu kuvaana na Majimaji saa 10.00 jioni.