TIMU ya vijana ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC U-20, inatarajia kushuka dimbani kesho Jumamosi saa 8.00 mchana, kuanza kufukuzia taji la Ligi ya Vijana (U-20 Uhai Cup) mwaka huu kwa kumenyana na Mtibwa Sugar.

Michuano hiyo itakayoanza kutimua vumbi kwenye viwanja vya Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), inadhaminiwa na Maji safi ya Uhai Drinking Water na Azam TV, ambapo jumla ya makundi manne yamepangwa.

Vijana hao wa Azam, wapo Kundi C sambamba na timu nyingine za Mtibwa Sugar, Mwadui na Majimaji, Kundi A likiwa na Yanga,Ruvu Shooting, Mbeya City na Mbao FC.

Kundi B lina timu za Simba, Singida United, Stand United na Njombe Mji, huku Tanzania Prisons, Lipuli, Kagera Sugar na Ndanda wakiunda Kundi D.

Tayari kikosi cha Azam U-20 kimeshawasili mkoani humo tokea jana Alhamisi usiku kikiwa na nyota wake kamili chini ya Kocha Mkuu, Meja Mstaafu Abdul Mingange na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar pamoja na Meneja wa timu hiyo, Luckson Kakolaki.

Kocha Mingange amekiandaa vilivyo kikosi hicho hadi kinaelekea kwenye michuano huku akiweka wazi kuwa amekwenda kupambana kuhakikisha wanatwaa taji hilo baada yam waka juzi kulikosa kwa kufungwa katika fainali na Simba, ambao ndio mabingwa watetezi.

Mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa ni kwenye mashindano yaliyopita katika hatua ya nusu fainali, Azam U-20 ikishinda kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya suluhu ndani ya dakika 120, wakati huo kikosi hicho kikifundishwa na Kocha Msaidizi wa sasa wa Azam FC, Idd Nassor Cheche.

Azam U-20 itakuwa na sura kadhaa kwenye michuano hiyo, wakiwemo washambuliaji wake tegemeo Paul Peter, Andrew Simchimba, Hamadi Azizi, pamoja na wachezaji wengine nahodha Ramadhan Mohamed, Abdul Omary, Said Issa, Lusajo Mwaikenda, Oscar Masai, Jamal Abdul, Tepsi Evance, Twaha Hashir, Omary Banda, Manzir Mwinyi, Gadafi Said.