MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shaaban Idd Chilunda, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Mei wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Chilunda ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Jacob Massawe wa Ndanda na Edward Shija wa Kagera Sugar katika uchambuzi uliofanywa wiki hii na kamati ya tuzo hizo.

Mshambuliaji huyo kinara wa mabao wa Azam FC msimu uliopita akifunga tisa VPL, ambapo katika mwezi huo aliisaidia timu hiyo kufunga mabao sita, kati ya hayo akifunga ‘hat trick’ timu yake ilipoilaza Tanzania Prisons mabao 4-1.

Kwa mwezi huo, Azam FC ilicheza michezo minne na kupata pointi tisa, ikishinda mitatu na kufungwa mmoja ikibaki katika nafasi yake ya pili na hakuwa na kadi yoyote.

Kwa upande wa Shija aliisaidia Kagera Sugar kupata pointi 10, akifunga mabao matatu katika michezo minne iliyocheza timu yake, ikishinda mitatu na kutoka sare mmoja na kupanda kutoka nafasi ya 12 iliyokuwepo mwezi Aprili hadi ya tisa.

Kutokana na ushindi huo, Chilunda atazawadiwa tuzo, kisimbuzi cha Azam TV na fedha taslimu Sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini Vodacom.

Wakati huo huo, mshambuliaji wa timu hiyo Yahya Zayd, ni miongoni mwa wachezaji 15 walioteuliwa kwenye orodha ya pili ya wachezaji wanaowania Tuzo ya Mchezaji Bora wa VPL msimu uliopita, sherehe za usiku huo wa tuzo mbalimbali za ligi zimepangwa kufanyika Juni 23, mwaka huu.

Wachezaji hao 15 ni miongoni mwa 30 waliotangazwa awali wiki mbili zilizopita kuwania tuzo hizo, ambapo watachujwa kulingana na takwimu mbalimbali za ligi hiyo na kubakia watatu.

Majina ya wachezaji hao watatu yanatarajiwa kutangazwa wiki ijayo, ambapo pamoja na  takwimu ambazo Kamati ya Tuzo inazo, pia itahusisha upigaji wa kura kutoka kwa wahariri wa habari za michezo, manahodha wa timu za Ligi Kuu pamoja na makocha wa timu za Ligi Kuu.

Wachezaji wengine 14 walioteuliwa naye ni mshambuliaji Obrey Chirwa, Papy Tshishimbi na Kelvin Yondani (Yanga),  Shafiq Batambuze, Mudathir Yahya na Tafadzwa Kutinyu (Singida United).

Wengine ni Adam Salamba (Lipuli), Habibu Kiyombo (Mbao), John Bocco, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na Erasto Nyoni (Simba), Marcel Kaheza (Majimaji) na Hassan Dilunga (Mtibwa).

Aidha licha ya Tuzo ya Mchezaji Bora wa VPL, pia siku hiyo katika sherehe zitakazofanyika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam kutatolewa tuzo mbalimbali ikiwemo ya Bingwa wa VPL, Mshindi wa Pili, Mshindi wa Tatu, Mshindi wa Nne na Mfungaji Bora.

Tuzo nyingine ni Timu yenye Nidhamu Bora, Mchezaji Bora wa Ligi ya Vijana (Tuzo ya Ismail Khalfan), Mchezaji Bora Chipukizi, Mwamuzi Msaidizi Bora, Mwamuzi Bora, Kipa Bora, Kocha Bora, Goli Bora, Kikosi Bora cha Msimu na Mchezaji wa Heshima.