BEKI chipukizi wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Abdul Omary ‘Hamahama’, ameongezewa mkataba wa miaka miwili zaidi kuendelea kuitumikia timu hiyo.

Hamahama, 19, ni zao la Azam Academy akilelewa tangu wakati kikosi hicho kikifundishwa na Vivek Nagul raia India, ambapo alipandishwa rasmi timu kubwa msimu ulioisha 2017/2018 na kufanikiwa kucheza mechi nne za mwisho za Azam FC kwa kiwango cha juu.

Wakati akipandishwa alipewa mkataba wa miaka miwili, na mechi za mwisho za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) alizocheza ni ile Azam FC iliyopoteza ugenini dhidi ya Stand United (2-1), nyingine ikizifunga Majimaji (2-0), Tanzania Prisons (4-1) na Yanga (3-1).

Zoezi la beki huyo kuingia mkabata mpya limesimamiwa na Meneja wa timu, Phillip Alando, ambaye wakati akiwa Meneja wa timu ndogo alishiriki kung’amua kipaji cha Hamahama, akimpendekeza kwa Kocha Nagul kabla ya kusajiliwa.

Aidha kwa kusaini mkataba huo mpya, beki huyo mfupi, mwenye spidi na uwezo wa kupiga krosi nzuri zenye madhara, kutamfanya kuendelea kuitumikia Azam FC hadi mwaka 2021.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB inayoongoza kwa ubora na usalama wa fedha zako nchini, maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, imejipambanua kwa kuwekeza vilivyo kwenye soka la vijana ikiwa na vikosi kuanzia umri chini ya miaka 11 hadi 20 (U-11 hadi U-20).

Kila msimu imekuwa na utaratibu wa kupandisha timu kubwa vijana wanaofanya vizuri, msimu uliopita ikiwatumia wanne akiwemo Hamahama, wengine wakiwa ni washambuliaji Yahya Zayd, Paul Peter na beki wa kati Oscar Masai.