MABINGWA watetezi wa michuano ya Kombe la CECAFA Kagame, Azam FC, wanatarajia kuanza kutetea ubingwa huo kwa kuvaana na Kator FC ya Sudani Kusini mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Juni 29 mwaka huu saa 10.00 jioni.

Azam FC ilitwaa ubingwa huo Agosti 2, 2015 hapa nchini wakati michuano hiyo ilipofanyika kwa mara ya mwisho, ikiifunga Gor Mahia mabao 2-0, yaliyofungwa na gwiji wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’, aliyehamia Simba msimu huu na Kipre Tchetche, anayecheza soka la kulipwa nchini Malaysia hivi sasa.

Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa kushirikiana na wenyeji Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadhamini Kampuni ya Azam TV wametoa ratiba muda mchache uliopita yenye makundi matatu, michuano ikitarajia kuanza Juni 29 hadi Julai 13 mwaka huu.

Makundi hayo yanaonyesha kuwa Azam FC ipo Kundi A sambamba na timu hiyo ya Sudan Kusini sambamba na timu nyingine mbili, JKU ya visiwani Zanzibar na Vipers ya Uganda, ambayo imeibuka mabingwa wa nchi hiyo msimu huu.

Mara baada ya Azam FC kufungua dimba na Kator, itashuka tena dimbani Julai Mosi kuvaana Vipers ya Uganda saa 1.00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex kabla ya kumalizia hatua ya makundi kwa kukipiga na JKU Julai 4 saa 1.00 usiku.

Kwa mujibu wa kanuni za michuano hiyo itakayoshirikisha timu 12, Katibu Mkuu wa CECAFA Nickolas Musonye, ameeleza kuwa timu mbili zitakazoongoza kila kundi zitafuzu kwa hatua ya robo fainali pamoja na timu bora mbili zilizoshika nafasi ya tatu zilizopata matokeo mazuri (best looser).

Bingwa wa michuano hiyo, anatarajia kuweka kibindoni kitita cha Dola za Marekani 30,000 (sawa na zaidi ya Sh milioni 62 za Tanzania), mshindi wa pili Dola 20,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 42 za Tanzania) na mshindi wa tatu Dola 10,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 22 za Tanzania).

Musonye amedokeza kuwa huenda kitita hiko kikaongezeka kama wadhamini wakijitokeza kwa wingi kudhamini mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya pili mfululizo jijini Dar es Salaam.

Wawakilishi wengine wa Tanzania, Simba na Yanga, wamepangwa Kundi C pamoja, wakiwa na St. George ya Ethiopia na Dakadaha ya Sonalia huku Kundi B likijumuisha Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Lydia Ludic (Burundi) na Ports (Djibout).

Kutokana na ujio wa michuano hiyo, likizo ya wachezaji wa Azam FC imefupishwa ambapo watarejea kuuanza msimu mpya (pre season) Juni 15 mwaka huu chini ya Kocha Mpya, Hans Van Pluijm.

Tujikumbushe 2015

Azam FC ilivyotwaa Kagame mwaka 2015, ilibeba kwa rekodi ya aina ya kutopoteza mchezo wowote wala kuruhusu bao katika mechi zote sita ilizocheza, ilianza kuzifunga KCCA (1-0), Al- Malakia (2-0) na Adama City (5-0) kwenye hatua ya makundi na kufuzu robo fainali.

Mabingwa hao wakaiongoa Yanga kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia suluhu ndani ya dakika 120, ikaifurusha KCCA kwa bao 1-0 kwenye nusu fainali kabla ya kuikung’uta Gor Mahia (2-0) katika fainali na kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza.