KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inayofuraha kuthibitisha kuwa imefanikiwa kumsajili kiungo Tafadzwa Kutinyu, kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongezwa kwa mujibu wa kiwango atakachoonyesha.

Kutinyu, 24, amekuwa na msimu mzuri tokea ajiunge na Singida United msimu huu iliyomsajili kutoka Chicken Inn ya nchini kwao Zimbabwe.

Ujio wa kiungo huyo ni sehemu ya kuboresha kikosi kwa mujibu wa ripoti ya benchi la ufundi kuelekea msimu ujao 2018/2019, baadaye mwezi huu Azam FC tukianza na patashika ya kutetea taji letu la CECAFA Kagame Cup tulilolitwaa mwaka 2015.

Kutinyu anakuwa ni mchezaji wa pili mpya kufikia makubaliano na Azam FC, wa kwanza akiwa ni mshambuliaji Donald Ngoma, ambaye amefikia makubaliano ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja.

Aidha msimu ujao benchi la ufundi la Azam FC litakuwa chini ya Mholanzi Hans Van Der Pluijm, ambaye muda wowote kuanzia kesho Jumatatu anatarajia kuingia rasmi mkataba wa kuinoa timu hiyo.

Tunawaomba mashabiki wetu wa Azam FC wawe watulivu katika kipindi hiki na kuendelea kuisapoti timu, kwani uongozi umejipanga kufanyia kazi ripoti ya benchi ya ufundi na kuboresha kikosi ili kusaka taji la ubingwa msimu ujao.

Ngoma huyoo Sauzi

Wakati huo huo, mshambuliaji Donald Ngoma anatarajia kuondoka nchini leo Jumapili saa 3.45 usiku na ndege ya Shirika la Kenya Airways kuelekea jijini Cape Town, Afrika tayari kufanyiwa vipimo vya afya ili kuona ni kwa kiasi gani majeraha yaliyokuwa yakimsumbua yamepona.

Ngoma ataongozana na Daktari wa timu, Dr. Mwanandi Mwankemwa, ambao kesho wanatarajia kuanza zoezi hilo la vipimo kwenye Hospitali ya Vincent Pallotti jijini humo.