NDOA ya miaka 10 kati ya nahodha wa Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’ na timu hiyo imefikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu, baada ya kiungo huyo kusaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Petrojet inayoshiriki Ligi Kuu nchini Misri.

Ninja amepokea baraka zote kutoka kwa Azam FC baada ya pande hizo mbili kufikia makubaliano ya kuondoka kwake, ambapo uongozi wa timu hiyo umemtakia kila la kheri katika maisha yake mapya ya kucheza soka la kulipwa.

Hadi anaamua kuondoka, Mao ni mmoja ya wachezaji aliyecheza kwa muda mrefu ndani ya timu hiyo akiungana na gwiji John Bocco ‘Adebayor’ (aliyehamia Simba), Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Agrey Moris, Mwadini Ally.

Safari yake ndani ya Azam FC ilianza tokea mwaka 2008 akianzia kwenye kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC ‘Azam FC Academy’ wakati huo akiwa mwanafunzi wa sekondari, alikuwa akicheza soka huku akiendelea na shule.

Kiungo huyo kiraka anayesifika kucheza kindava na kuharibu mbinu za wapinzani, amepitia historia ndefu ndani ya timu hiyo tokea akiwa ngazi ya chini ya Azam Academy, akiwa kama nahodha aliiongoza kutwaa ubingwa wa michuano ya vijana ‘Uhai Cup’ mara mbili mfululizo.

Katika historia yake ya maisha ya soka, Himid ameweza kuwa kiongozi uwanjani kama nahodha wa vikosi vyote vya timu za Taifa za Vijana (U-17 hadi U-23) hadi za wakubwa na vilevile kuanzia msimu hadi anaamua kuondoka amekuwa nahodha wa Azam FC.

Rekodi Azam FC                                         

Kiungo huyo hadi anaondoka Azam FC, amefanikiwa kucheza jumla ya mechi rasmi 246 za mashindano mbalimbali, za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzani Bara (VPL) zikiwa 179, CECAFA Kagame Cup (8), Mapinduzi Cup (29), Kombe la ASFC (10), Ngao ya Jamii (5).

Mbali na mechi hizo, akiwa anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji pekee wa Azam FC aliyecheza mechi zote za mashindano ya Afrika (CAF Club Competition), akiwa amecheza jumla ya michezo 15, mechi mbili zikiwa za Ligi ya Mabingwa Afrika na 13 za Kombe la Shirikisho Afrika.

Himid ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa Taifa Stars na Pamba ya Mwanza, Mao Mkami ‘Ball Dancer’, ametwaa jumla ya mataji saba rasmi akiwa na Azam FC, taji moja ya Ligi Kuu msimu 2013/2014, timu hiyo ikilitwaa kwa rekodi ya kutofungwa mchezo wowote.

Mataji mengine aliyobeba ni Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) mwaka 2015, ikilibeba kwa rekodi ya aina yake ya kutopoteza wala kuruhusu nyavu zake kutikiswa hadi sasa ikiwa ndio bingwa mtetezi wa taji hilo, pia ametwaa Kombe la Mapinduzi mara nne na Ngao ya Jamii mara moja.

Msimu uliopita alitwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Azam FC (NMB Player Of The Month) mwezi October-November.

Himid kwa Azam FC

Nahodha huyo alitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuiaga familia yote ya Azam FC , akiwashukuru makocha, viongozi na wafanyakazi wote kwa kazi kwa pamoja na ushirikiano kwa kipindi chote alichokuwa hapo.

“Asante Mungu kwa kumaliza msimu salama, asante kwa technical staff, makocha, viongozi na wafanyakazi wote wa @azamfcofficial kwa kufanya kazi pamoja kila siku kwa ushirikiano katika kupanda na kushuka, huzuni na furaha na bado mlikua bega kwa bega na mimi miaka yote, ni huzuni kusema kwaheri lakini haikua na jinsi nilishafanya maamuzi.

“Na kushirikiana na uongozi wa Azam FC mkaniruhusu nilipoomba ruhusa ya kutafuta changamoto mpya, nimeishi kama mwanafamilia kwa miaka yote nilikuja nikiwa kijana mdogo kabisa wa kidato cha kwanza naondoka nikiwa nimepevuka kimwili na kiakili, mimi ni binadamu kama kuna sehemu niliwakosea naombeni mnisamehe na mimi nimesamehe kama mlinikosea.
asanteni sana na kila la kheri katika misimu inayokuja,” aliaga Himid Mao.

Azam FC tunachukua fursa hii kumshukuru kwa muda wote aliokuwa nasi na tunauheshimu mchango wake kwa kiasi kikubwa kwa mafanikio aliyoshiriki na tunapenda kumtakia kila la kheri katika maisha yake mapya ya soka.

Nafasi hiyo ikawe chachu kwake ya kusogea mbele zaidi ya hapo, na tunaamini kwa jitihada zake binafsi atakifikia kule anapotarajia kufika. #ThanksForHistoryHimid Mao23