UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, unathibitisha kuwa kikosi hicho kinatarajia kufundishwa na Mholanzi Hans Van Pluijm, kuanzia msimu ujao.

Pluijm ambaye anaifundisha Singida United hivi sasa akiwa tayari ameaga kutoendelea nao msimu ujao, anakuja Azam FC kuchukua mikoba ya Mromania Aristica Cioaba, aliyekuwa na kikosi hicho msimu uliopita.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Jaffar Idd, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa Mholanzi huyo ataungana na Azam FC mara baada ya kumalizia kibarua cha Fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar keshokutwa Jumamosi.

“Kwa sasa tumeamua kumtangaza baada ya kukubaliana naye kila kitu, mambo mengine tutayaweka wazi Jumatatu ijayo, na kingine kuanzia msimu ujao Azam FC itakuwa kampuni ikijulikana Azam FC Company Limited,” alisema.

Azam FC inaamini ya kuwa Pluijm ana uzoefu wa kutosha wa soka la Kimataifa na Tanzania utakaoisaidia timu hiyo, akizifundisha kwa mafanikio Singida United na Yanga aliyeipa mataji ya ligi, FA Cup na kuifikisha hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kabla ya kutua Yanga, Pluijm aliwahi kuzifunza Ashanti Gold, Medeama na Berekum Chelsea zote za Ghana.

Wakati huo huo, Idd alisema kuwa msimu ujao timu hiyo itakuwa bila Nahodha wake na mchezaji wa muda mrefu, Himid Mao ‘Ninja’, ambaye ameomba ruhusa ya kwenda kusakata kabumbu nje ya nchi.

“Uongozi sisi hatuna kipingamizi, Himid ni mchezaji wetu wa muda mrefu tokea akiwa mdogo kabisa ameshiriki mafanikio mengi ya timu, mara baada ya kuleta maombi hayo sisi tulimkubalia na tunamtakia kila la kheri huko aendako katika maisha yake mapya,” alisema.