WACHEZAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, wamepewa mapumziko ya siku 35 hadi Julai 3 mwaka huu watakaporipoti kuanza maandalizi ya msimu ujao.

Azam FC imefunga msimu jana kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Yanga, ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1 na kujihakikisha kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Simba kwa pointi 58.

Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa wachezaji wote watakaosajiliwa na waliopo kikosini hivi sasa wanatakiwa kuripoti Julai 3 kwa ajili ya kuanza mchakamchaka wa maandalizi ya msimu ujao 2018-2019.

“Tutakaporejea tutafanya maandalizi kwa siku kadhaa kabla ya kuelekea nchini Uganda tulipofanya maandalizi ya msimu uliomalizika (pre season) ambapo huko tutacheza mechi kadhaa za kirafiki kama tulivyofanya msimu uliopita kabla ya kurejea nchini,” alisema.

Azam FC ikiwa nchini Uganda kujiandaa na msimu ulimalizika ilicheza mechi tano za kirafiki, ikitoka sare dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ (2-2), KCCA (1-1), ikazinyuka URA (2-0), Onduparaka (3-0) na Vipers (1-0).