KIPA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Mwadini Ally, ameongeza mkataba mpya wa mwaka mmoja kuendelea kuitumikia timu hiyo.

Mwadini amekuwa na kiwango kizuri msimu huu katika mechi zote alizocheza, jambo ambalo limeshawishi benchi la ufundi kupendekeza aongezewe mkataba mpya.

Akithibitisha taarifa hiyo, Meneja wa timu hiyo, Phillip Alando, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa kipa huyo amefanya kazi kubwa langoni kwa mechi chache alizocheza jambo ambalo limewashawishi kumpa mkataba huo.

“Kutokana na kiwango alichokionyesha kwa baadhi ya mechi alizocheza Azam FC imeona imuongezee mwaka mmoja zaidi katika kuitumikia klabu,” alisema.

Aliongeza kuwa mbali na kuifanyia mazuri timu, pia kipa huyo amekuwa hana makuu na mhimili mkubwa kwa wachezaji vijana wanaochipukia hasa makipa.

Mwadini katika mechi saba alizodaka msimu huu kwenye mashindano yote (sawa na dakika 630) ameruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu tu.

Kutokana na kiwango chake bora, alichaguliwa na mashabiki kuwa Mchezaji Bora wa klabu (NMB Player Of The Month) kwa mwezi wa Machi.