BODI ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imefanya mabadiliko ya muda kwenye mchezo wa ligi kati ya Azam FC na Tanzania Prisons utakaofanyika kesho Jumapili, ambapo hivi sasa umepangwa kuanza saa 2.00 usiku katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Awali mchezo huo ulikuwa umepangwa kuanza saa 1.00 usiku, lakini kutokana na kuanza kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, TPLB imeona ni busara kupeleka muda kidogo mbele ili kuwapa nafasi Waislamu kufutari kabla ya mtanange kuanza.

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye maandalizi makali kuelekea mchezo huo, ambapo leo usiku kitafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuvaana na Wanajeshi hao, ambao waliwapa kipigo cha mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza.

Tayari Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche ameshaweka wazi kuwa amekipanga kikosi chake kuendeleza ubabe dhidi ya Tanzania Prisons huku akikiri mchezo kuwa na ushindani na burudani kwa mashabiki watakaohudhuria.

“Tunajipanga tofauti na vile tulivyojipanga kwenye mchezo wa mwanzo, kwa sababu mwanzoni tulicheza uwanja tofauti na tulikuwa na baadhi ya wachezaji ambao sasa hivi hawapo, lakini sasa hivi tunajipanga kivingine kuhakikisha tunaendeleza ubabe wetu,” alisema Cheche mwanzoni mwa wiki hii alipokuwa akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz

Mabingwa hao wa ligi msimu 2013/2014 bila kufungwa mchezo wowote, wanaingia dimbani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa 2-0 walioupata dhidi ya Majimaji kwenye mtanange uliopita huku Prisons ikitoka suluhu na mahasimu wao Mbeya City katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Azam FC ipo kwenye vita kali ya kuwania nafasi ya pili kwenye ligi, hadi sasa ikiwa inaishikilia baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 52, Yanga yenye mechi mbili mkononi ikiwa nazo 48.

Rekodi zilizopita

Mchezo wa kesho utakuwa ni wa 16 kwa timu hizo kukutana kwenye ligi kihistoria, katika mechi 15 zilizopita Azam FC imeshinda mara sita, Prisons imeibuka kidedea mara tatu na mechi sita zikiisha kwa sare.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana katika dimba hilo la Azam Complex, Azam FC ilishinda bao 1-0 lililofungwa na gwiji wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’, aliyehamia Simba msimu huu.

Jumla ya mabao 24 yamefungwa na timu hizo katika mechi zote 15 walizokutana, Azam FC imefunga 14  na Prisons ikitupia 10 tu kwenye nyavu za matajiri hao, ambao msimu huu wametwaa taji la Mapinduzi Cup.