KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefikia makubaliano ya kuachana na mshambuliaji wake, Bernard Arthur mwishoni mwa msimu huu.

Arthur alisajiliwa kwenye dirisha dogo lililiopita la usajili akitokea Liberty Professional ya kwao Ghana, kuziba nafasi ya mshambuliaji mwingine kutoka huko Yahaya Mohammed, ambaye amerejea Aduana Stars.

Azam FC imeamua kufikia makubaliano na mshambuliaji, baada ya Arthur mwenyewe kuomba aruhusiwe kuondoka mwishoni mwa msimu ili akasake maisha sehemu nyingine, ambapo baada ya maafikiano uongozi wa timu hiyo umeamua kumruhusu.

Hivyo, mshambuliaji huyo, 21, ataendelea kusalia hadi msimu huu utakapomalizika Mei 28 mwaka huu, Azam FC itakapocheza mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Yanga.

Hadi anafikia uamuzi huo, Arthur mpaka sasa amecheza jumla ya dakika 937 (sawa na mechi 10 na dakika 37), zikiwa ni mechi za mashindano na za kirafiki, akifunga jumla ya mabao sita.

Mchanganuo wa mabao hayo sita, matatu amefunga mashindanoni (moja Kombe la Mapinduzi na mawili VPL) na mengine yaliyobakia akifunga katika mechi za kirafiki (mawili vs Villa Squad, moja vs Friends Ranger).

Uongozi wa Azam FC unamshukuru Arthur kwa muda wote alioutumia kuitumikia timu hiyo na unamtakia kila la kheri kwenye timu yake mpya anayokwenda.