KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imedhihirisha kuwa inataka kumaliza kwenye nafasi mbili za juu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu baada ya usiku wa kuamkia leo Jumamosi kuiadhibu Majimaji mabao 2-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 52 ikiwa nafasi ya pili zilizoifanya kuzidi kuikimbia Yanga kwa pointi nne ikishika nafasi ya tatu na mechi tatu mkononi huku Simba ikiwa tayari imetangaza ubingwa ikiwa na pointi 65 kileleni.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, licha ya kutengeneza nafasi nyingi za kufunga kipindi cha kwanza ilibidi isubiri hadi kipindi cha pili kuweza kuandikisha ushindi huo muhimu.

Mabao hayo muhimu yaliwekwa kimiani na mshambuliaji Shaaban Idd, dakika ya 49 akiunganisha kwa shuti la kiufundi pasi safi ya juu aliyopigiwa na straika mwenzake, Yahya Zayd.

Shaaban alihusika pia katika bao la pili la Azam FC, safari hii akifanyiwa madhambi pembeni kidogo ya eneo la 18, ambapo kiungo Frank Domayo, alitumia vema nafasi hiyo dakika ya 58 kwa kuandika bao safi la mkwaju wa adhabu ndogo ya moja kwa moja.

Mabingwa hao wa ligi msimu 2013/2014, kuelekea dakika 25 za mwisho za mchezo walifanya mabadiliko kadhaa yaliyozidi kuongeza kasi eneo la ushambuliaji, hasa ingizo la mshambuliaji, Mbaraka Yusuph, aliyeingia na nguvu mpya na kuipa wakati mgumu safu ya ulinzi ya Majimaji dakika zote hadi pambano hilo linamalizika.

Kwa mujibu wa rekodi, huo unakuwa mchezo wa 10 kwa timu hizo kukutana kwenye ligi, Azam FC ikiwa imeshinda jumla ya mechi sita huku mechi nne zikiisha kwa sare.

Kabla ya kuanza mchezo huo, lilifanyika zoezi la ugawaji tuzo kwa wachezaji bora wa mwezi wa Azam FC kwa timu ndogo na kubwa, ambapo kipa Mwadini Ally, alipokea kwa timu kubwa (NMB Player Of The Month) na Abdul Haji Omary, alipata naye kwa upande wa timu ndogo (Uhai Player Of The Month).

Abdul amekuwa kwenye kiwango kizuri akiwa na timu ndogo, hali iliyopelekea hivi sasa kutumika timu ya wakubwa akiwa ameanzishwa mechi mbili mfululizo za Azam FC akicheza kwa dakika zote 90, akionekana kufanya vema huku krosi zake nyingi zikiwa na madhara.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kurejea tena mazoezini Jumatatu ijayo jioni tayari kuanza maandalizi ya kuikabili Tanzania Prisons, mtanange utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC leo:

Mwadini Ally, Abdul Omary, Bruce Kangwa, David Mwantika, Abdallah Kheri/Braison Raphael dk 88, Himid Mao (C), Joseph Mahundi, Frank Domayo, Shaaban Idd, Yahya Zayd/Mbaraka Yusuph dk 63, Ramadhan Singano/Masoud Abdallah dk 76