KIPA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Mwadini Ally, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa timu hiyo (NMB Player Of The Month) mwezi Machi.

Mwadini ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwa na kiwango kizuri mwezi huo akicheza jumla ya mechi nne (sawa na dakika 360) akiruhusu wavu wake kutikiswa mara moja tu.

Kipa huyo amevuna asilimia 52 za kura 1,000 zilizopigwa na mashabiki wa soka kwenye ukurasa wa mtandao wetu wa facebook, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ amevuna asilimia 25 huku Frank Domayo ‘Chumvi’ naye akivuna asilimia 23 ya kura hizo.

Hii ni mara ya kwanza kwa kipa huyo mzaliwa wa Unguja, visiwani Zanzibar kubeba tuzo hiyo, ambapo hadi hivi sasa wengine waliotwaa msimu huu ni Yakubu Mohammed, Mbaraka Yusuph, Himid Mao ‘Ninja’, Razak Abalora na Yahya Zayd.

Tunampongeza Mwadini kwa kutwaa tuzo na mashabiki wote walioshiriki kupiga kura.