HAIJAWA siku nzuri leo kwa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, baada ya kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga.

Bao lililofungwa na beki wa Stand United, Ally Ally, kwenye dakika za nyongeza liliondoa uwezakano wa Azam FC kuondoka na pointi moja ugenini, kufuatia awali mshambuliaji Shaaban Idd, kusawazisha bao dakika ya 76 akifuta lile la uongozi la wenyeji hao lililofungwa dakika ya 45 na Sixtus Sabilo.

Azam FC ilifanya jitihada za kufunga mabao kwa nyakati tofauti kupitia kwa wachezaji wake, Shaaban Idd, Yahya Zayd, Frank Domayo kwenye mchezo huo lakini safu ya ulinzi ya Stand United ilisimama vema.

Dakika ya 62 beki wa Azam FC, Abdallah Kheri, aliruka juu na kupiga kichwa kizuri lakini kilitoka sentimita chache ya lango la Stand, Sebo alipiga kichwa hicho akiunganisha kona iliyochongwa vizuri na Joseph Mahundi.

Huo ni mchezo wa tatu Azam FC inapoteza ugenini baada ya awali kufungwa zingine dhidi ya Simba (1-0) na Ruvu Shooting (2-1), takwimu zinaonyesha kuwa hadi sasa mabingwa hao wameshinda jumla ya mechi 13, sare 10 na kupoteza nne.

Baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kesho Jumatatu alfajiri kitaanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam tayari kuanza maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Majimaji utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Ijumaa ijayo saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC leo:

Mwadini Ally, Abdul Omary, Bruce Kangwa, David Mwantika, Abdallah Kheri, Himid Mao (C), Joseph Mahundi/Braison Raphael dk 73, Frank Domayo, Shaaban Idd/Bernard Arthur dk 85, Yahya Zayd, Ramadhan Singano/Idd Kipagwile dk 61