KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imebakiza dakika 360 tu (sawa na mechi nne) kuweza kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu, ambapo imejinasibu kupambana kushinda mechi zote.

Kwa mujibu wa Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, alipozungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz amesema kuwa wamejiwekea  malengo hayo ili kulinda heshima na kujiweka pazuri kwenye msimamo wa ligi.

“Matarajio yetu sisi ni kufanya vizuri kwenye mechi zote nne zilizobaki ili kuhakikisha tunaweka heshima yetu na kujiweka sawa kwenye ligi, tutafanya hivyo kwa kufanya mazoezi vizuri, tutapunguza makossa kwenye mechi na kuongeza mazuri na kuhakikisha kila anayekuja mbele yetu tunamfunga,” alisema.

Katika mechi hizo nne ambazo Azam FC imebakisha, itaanza keshokutwa Jumapili kwa kukipiga na Stand United kabla ya kurejea nyumbani kumalizia mechi tatu dhidi ya Majimaji (Mei 11), Tanzania Prisons (Mei 18) na Yanga (Mei 28).

Kikosi cha Azam FC tayari kimewasili mkoani Shinyanga tokea usiku wa kuamkia leo kikiwa tayari kabisa kukabiliana na Stand kwenye Uwanja wa Kambarage, katika mchezo unaotarajia kuwa mkali na wa aina yake.

Akizungumzia mchezo huo baada ya kwenye raundi ya kwanza kuichapa timu hiyo mabao 3-0, Cheche alisema kuwa mchezo utakuwa mgumu lakini akajinasibu ya kuwa watapambana vilivyo kuondoka na pointi zote tatu.

“Mchezo bado utakuwa mgumu kwa sababu kila timu inayokutana na Azam basi hujiandaa vizuri, sio kwamba timu ukiifunga leo kwamba haijui nafikiri mchezo utakuwa mgumu na wa ushindani zaidi ya ule tuliocheza na Mtibwa (Jumamosi iliyopita) na vijana nimeshaambia hilo ili kuweka umakini,” alisema.

Naye Nahodha wa Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, alisema kuwa wataingia uwanjani kufuata mbinu za kocha huku akiwaambia mashabiki watapigania kupata matokeo mazuri uwanjani kwa kujitolea kwa asilimia 100.

“Sisi kwa upande wetu tutajitolea kadiri tunavyoweza uwanjani kwa asilimia 100 ili timu iweze kupata matokeo, mashabiki waendelee kuisapoti timu bila kujali matokeo gani yanapatikana lakini umoja wetu unaweza kutusababisha kupata matokeo mazuri mfululizo na tunapoachana kidogo tunatoa nafasi ya kutopata matokeo mazuri,” alisema.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, hadi sasa kwenye msimamo wa ligi inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 49 nyuma ya Simba iliyokileleni kwa pointi 62 na Yanga yenye mechi mbili mkononi katika nafasi tatu ikiwa nazo 48.