NYOTA watatu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kipa Mwadini Ally ‘Reina’, viungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Frank Domayo ‘Chumvi’, wamechaguliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Azam FC (NMB Player Of The Month) mwezi Machi.

Mwezi huo Azam FC imecheza jumla ya mechi nne ikishinda za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Singida United (1-0), Mwadui (1-0) na Mbao (2-1), huku ikipoteza walipokipiga na Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) kwa mikwaju ya penalti 9-8 kufuatia dakika 90 kumalizika kwa suluhu.

Wachezaji hao watatu walikuwa kwenye kiwango kizuri mwezi huo, wakicheza mechi zote hizo kwenye ligi na Azam FC ikivuna pointi zote tisa huku Mwadini akiruhusu nyavu zake kuguswa mara moja tu ndani ya dakika 270 (sawa na mechi tatu).

Tuzo hiyo inadhaminiwa na wadhamini wakuu wa Azam FC, Benki ya NMB inayoongoza kwa sasa nchini, ambapo mpaka hivi sasa tokea ianzishwe msimu huu imeshachukuliwa na wachezaji watano ambao ni Yakubu Mohammed, Mbaraka Yusuph, nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Razak Abalora na Yahya Zayd.

Mbali na mshindi kupewa tuzo maalumu, benki hiyo pia imeanza kutoa kitita cha Sh. 500,000 kwa bingwa atakayeibuka kidedea, ambaye atapatikana kwa kupigiwa kura na mashabiki kwenye ukurasa maalum wa katika mtandao wa facebook.

Mwisho wa zoezi la kupiga kura kwa mashabiki ni Jumanne ijayo saa 6.00 mchana kabla ya bingwa kutangazwa.

Anza kupiga kura yako kwa kubofya hapa <<<< https://poll.fbapp.io/nmb-player-of-the-month-march >>>>