KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imesogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya jioni hii kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.

Azam FC imepanda hadi nafasi hiyo baada ya kufikisha jumla ya pointi 49 ikiizidi Yanga kwa pointi moja ambayo ina mechi tatu mkononi ikiwa imecheza mechi 23 na matajiri hao 26.

Bao pekee la Azam FC limefungwa kiustadi na mshambuliaji Shaaban Idd, dakika ya 39 akiunganisha kona iliyochongwa na Ramadhan Singano ‘Messi’, kona hiyo ilitokana na kipa wa Mtibwa, Shaaban Kado, kuipangua faulo nzuri iliyopigwa na nahodha msaizidi, Agrey Moris.

Mabingwa hao wa VPL msimu wa 2013/2014 walifanikiwa kucheza vema kipindi cha kwanza cha mchezo huo wakifanikiwa kutengeneza nafasi takribani tano za kufunga mabao kabla ya Shaaban kuipa bao hilo muhimu lililodumu hadi kumalizika kwa pambano hilo.

Safu ya ulinzi ya Azam FC chini ya Moris, Abdallah Kheri, kwenye beki ya kati na wale wa pembeni, Bruce Kangwa, Swaleh Abdallah, wakishirikiana na viungo nahodha Himid Mao ‘Ninja’ na Frank Domayo ‘Chumvi’, waliweza vilivyo kuwabana wachezaji wa Mtibwa, ambao walikuja juu kipindi cha pili ili kusawazsiha bao.

Langoni kipa wa Azam FC, Mwadini Ally, aliweza kuibuka shujaa wa mchezo, akifanya kazi kubwa kuokoa michomo mingi ya Mtibwa ikiwemo faulo ya hatari iliyopigwa kipindi cha pili na mshambuliaji wa Mtibwa, Kelvin Sabato.

Winga Singano mbali na kutoa pasi ya bao alifanikiwa kuonyesha kiwango kizuri kwenye mchezo huo akiichachafya vilivyo safu ya ulinzi ya Mtibwa.

Kwa matokeo hayo, rekodi ya Azam FC inaendelea kuimarika dhidi ya Mtibwa, katika mechi 20 walizocheza za ligi, matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex wameshinda mara 10, Mtibwa akifanya hivyo mara mbili na mechi nane wakienda sare.

Baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitashuka tena dimbani Mei 6 mwaka huu, kuvaana na Stand United mchezo utakaofanyika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC leo:

Mwadini Ally, Swaleh Abdallah, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Agrey Moris, Himid Mao (C), Joseph Mahundi/Braison Raphael dk 70, Frank Domayo, Shaaban Idd/Mbaraka Yusuph dk 77, Yahya Zayd, Ramadhan Singano/Idd Kipagwile dk 82