MCHEZO kati ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC na Mtibwa Sugar umefanyiwa mabadiliko ya muda, ambapo sasa utafanyika Uwanja wa Manungu, Turiani Morogoro, kesho Jumamosi saa 10.00 jioni.

Awali mchezo huo ulikuwa ufanyike saa 8.00 mchana, lakini Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imeamua kuusogeza hadi jioni kutokana na ratiba ya wadhamini wa matangazo ya televisheni Azam TV kutobana muda huo.

Tayari kikosi cha Azam FC kimewasili mkoani Morogoro tokea jana saa 12 jioni kikiwa tayari kuvaana na Wakatamiwa hao, ambapo jioni ya leo kitafanya mazoezi ya mwisho kujiweka sawa na mchezo huo.

Timu hizo zimekuwa na upinzani mkali mara zote zinapokutana, katika rekodi zimecheza mechi 19 za ligi, Azam FC ikiwa imeshinda mara tisa, Mtibwa Sugar mara mbili huku mechi nane zikiisha kwa sare, ambapo hivi sasa inasubiriwa kuona namna matokeo yatakavyokuwa katika mechi yao ya 20 ya ligi.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye ligi ilikuwa ni Novemba 27 mwaka jana, zikitoka sare ya bao 1-1, Azam FC ikitangulia kufunga kupitia kwa winga Enock Atta kabla ya Kelvin Sabato kuisawazishia Mtibwa Sugar kwa mkwaju wa moja kwa moja wa adhabu ndogo.

Azam FC itamkosa Kocha Mkuu wake, Aristica Cioaba, ambaye amesimamishwa na Kamati ya Saa 72, kufuatia kuondolewa kwenye benchi na mwamuzi Jonesia Rukyaa, katika mchezo uliopita dhidi ya Njombe Mji ulioisha kwa suluhu.

Nahodha Msaidizi, Agrey Moris, atarejea tena kikosini baada ya kumaliza adhabu ya kutocheza mchezo mmoja kufuatia kadi nyekundu iliyotokana na kadi mbili za njano aliyopata kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ulioisha kwa Azam FC kupoteza kwa mabao 2-0.

Kikosi cha Azam FC kimejipanga kufanya vizuri katika mchezo huo na kuondoa rekodi mbaya ya kutoshinda katika mechi tatu zilizopita, ikipata suluhu mbili dhidi ya Mbeya City na Njombe Mji na kufungwa mmoja.

Hadi sasa kwenye msimamo wa ligi, Azam FC inayodhaminiwa na Maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB inayoongoza kwa sasa ikiwa na matawi Tanzania nzima na Tradegents, inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 46 huku wapinzani wao Mtibwa Sugar ikiwa nafasi ya sita kwa pointi 33.