KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, muda mchache ujao saa 8 mchana kinatarajia kuanza safari ya kuelekea mkoani Morogoro, tayari kusaka pointi tatu muhimu dhidi ya Mtibwa Sugar keshokutwa Jumamosi.

Azam FC inaondoka ikiwa imemaliza programu ya mazoezi ya mwisho jijini Dar es Salaaam leo asubuhi kikiwa fiti kabisa kusaka ushindi huo muhimu kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Katika kujiandaa vilivyo na mchezo huo, juzi kikosi hicho kilicheza mchezo wa kujiweka sawa dhidi ya Kombaini ya Jeshi na kushinda mabao 2-0 yaliyofungwa na mshambuliaji Shaaban Idd na winga Enock Atta.

Nahodha Msaidizi wa Azam FC, Agrey Moris, aliyekosa mchezo uliopita dhidi ya Njombe Mji akitumikia adhabu ya kadi nyakundu (njano mbili), atarejea kikosini kuimarisha eneo la ulinzi ambapo kwa sasa anashirikiana vema na Abdallah Kheri Sebo, aliyeendelea kuonyesha uwezo mkubwa.

Timu hizo zilipokutana kwenye raundi ya kwanza katika viunga vya Azam Complex, zilitoka sare ya bao 1-1, Azam FC ikitangulia kufunga kupitia kwa winga Enock Atta kabla ya Kelvin Sabato kusawazisha dakika za mwisho kwa mpira wa moja kwa moja wa adhabu ndogo.

Aidha timu hizo zilikutana tena kwenye robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) mwezi uliopita na Azam FC kupoteza kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 9-8 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suhulu, mchezo ukifanyika Uwanja wa Azam Complex.

Hadi sasa kwenye msimamo wa ligi, Azam FC inayodhaminiwa na Maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB inayoongoza kwa sasa ikiwa na matawi Tanzania nzima na Tradegents, inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 46 huku wapinzani wao Mtibwa Sugar ikiwa nafasi ya sita kwa pointi 33.