KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeichapa Kombaini ya Jeshi mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye viunga vya Azam Complex jioni ya leo.

Mchezo huo ulikuwa ni mahususi kwa ajili ya kikosi cha mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi mara mbili mfululizo, kujiweka sawa kabla ya kwenda kucheza na Mtibwa Sugar kwenye mtanange wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Manungu Jumamosi hii.

Mabao ya Azam FC yamewekwa kimiani katika kila kipindi cha mchezo huo na mshambuliaji Shaaban Idd, aliyefunga la kwanza kabla ya winga Enock Atta kupiga la pili mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Benchi la ufundi la Azam FC liliwapa nafasi ya kucheza wachezaji wote katika mchezo huo wakiwemo nyota waliopandishwa mabeki Lusajo Mwaikenda, Oscar Masai na Abdul Omary walioingia kipindi cha pili na kuonekana kufanya vema.