KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kucheza dhidi ya Kombaini ya Jeshi katika mchezo wa kirafiki unaotarajia kufanyika kwenye uwanja nyasi za kawaida ndani ya Azam Complex kesho Jumanne saa 10.00 jioni.

Mchezo huo ni mahususi kabisa kwa ajili ya benchi la ufundi la Azam FC kuwapima wachezaji wa timu hiyo kulingana na mafunzo waliyowapa wiki nzima kabla ya kuvaana na Mtibwa Sugar Jumamosi hii kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Kikosi cha Azam FC kinachodhaminiwa na Benki ya NMB, maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, kipo kwenye maandalizi makali kuelekea mchezo huo muhimu wa ligi utakaofanyika Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, ambapo kimejipanga kufanya vizuri na kurekebisha makosa ya kutopata ushindi katika mechi tatu zilizopita.

Hadi sasa Azam FC imejikusanyia jumla ya pointi 46 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo kikizidiwa pointi mbili na Yanga iliyonafasi ya pili na mechi mbili mkononi huku Simba yenye mechi moja mkononi ikiwa kileleni kwa pointi 56.

VIDEO LINK <<<< https://youtu.be/JdB86IQAwO0 >>>>