BEKI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, David Mwantika, ameanza rasmi mazoezi ya wenzake wiki hii ikiwa baada ya kuugua ghafla uwanjani wiki tatu zilizopita.

Mwantika alipata hitilafu hiyo ya mwili dakika ya 65 wakati Azam FC ikicheza hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Mbagala Zakhem na kuhamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke, na baadaye ile ya Rufaa ya Muhimbili (MNH).

Baada ya kuhamishiwa Muhimbili na kutibiwa vema kabisa, iliwalazimu madaktari wa hospitali hiyo kumhamishia kitengo cha magonjwa ya moyo cha Taasisi ya Jakaya Kikwete na kufanyiwa vipimo ili kujua kama ana tatizo la aina hiyo.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, alisema kuwa tayari wamepokea majibu ya vipimo hivyo vinavyoonyesha kuwa beki huyo hana tatizo la moyo akidai yupo fiti kabisa na ndio maana wamemruhusu kuanza mazoezi mepesi.

“Mwantika alipata huduma Muhimbili na akalazwa katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete na baada ya kufanyika uchunguzi wa kina kabisa na vipimo vya kina na kuangalia mishipa ya damu ya moyo imethibitika kwamba Mwantika hana tatizo la moyo.

“Na sasa amerudi tena na katika siku mbili hizi tulianza kuangalia uwezo wake wa kukimbia na uwezo wake wa pumzi kwa hiyo alianza mazoezi ya kukimbia kwa dakika 20, dakika 30 na leo (jana) amekimbia dakika 45,” alisema.

Mwankemwa alisema kuwa wiki ijayo beki huyo ataruhusiwa kuanza mazoezi ya kawaida na wenzake tayari kabisa kurejea katika ushindani.

Yakubu Mohammed je?  

Akizungumzia maendeleo ya beki Yakubu Mohammed, aliyevunjika mfupa mdogo wa mguu wa kulia (fibula),  Mwankemwa alisema licha ya wiki nne kupita na kuondolewa hogo (P.O.P) bado beki huyo anasikia maumivu kwenye eneo hilo.

Daktari huyo alisema kutokana na hali hiyo, beki huyo atalazimika kwenda nchini Afrika Kusini kufanyiwa uchunguzi zaidi kati ya Jumatano au Alhamisi ya wiki ijayo ili kujua tatizo linalomkabili.

“Baada ya kutolewa P.O.P imeonekana bado ule mguu una maumivu makali sana kwa hiyo uongozi uliamua kwamba aende naye akafanyiwe uchunguzi Afrika Kusini kwa hiyo Jumatatu inayokuja (kesho) tutafanya taratibu za kutafuta Visa na Yakubu kama sio siku ya Jumatano ijayo au Alhamisi atakwenda kwa ajili ya matibabu Afrika Kusini,” aliongeza Mwankemwa.

Kikosi cha Azam FC kinachodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, kwa sasa kinaendelea na mazoezi ya kawaida kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro Jumamosi ijayo saa 10.00 jioni.

Kupata ripoti kamili ya Daktari wa Azam FC, fungua link hii chini:

<<<<https://youtu.be/fQ7LvAN8XJU>>>>