KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeshindwa kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kulazimishwa suluhu na Njombe Mji, mchezo uliomalizika usiku huu katika Uwanja wa Azam Complex.

Ushindi wowote wa Azam FC leo ungeifanya kusogea hadi nafasi ya pili ikiishusha Yanga, ambayo ingerejea nafasi yake hiyo itakapopata matokeo mazuri kwenye mechi zake tatu za viporo.

Safu ya ushambuliaji ya Azam FC iliyokuwa ikiongozwa na Bernard Arthur na Yahya Zayd, itabidi ijilaumu yenyewe baada ya kukosa mabao mengi ya wazi katika kila kipindi yaliyoinyima timu hiyo ushindi.

Kwa kiasi kikubwa Azam FC iliweza kutawala kipindi cha kwanza na kutengeneza nafasi za wazi takribani sita lakini ubutu wa eneo la ushambuliaji ulipelekea kushindwa kupata matokeo waliyoyahitaji na kuifanya Njombe Mji kupata pointi ugenini.

Dakika ya 27 Nahodha wa Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, alikosa penalti baada ya kipa wa Njombe kudaka mpira alioupiga, mkwaju huo ulitokana na winga Ramadhan Singano ‘Messi’ kufanyiwa madhambi kwenye eneo la 18.

Katika mchezo huo, benchi la ufundi la Azam FC lililazimika kumtumia nahodha Himid Mao ‘Ninja’, kama beki wa kati kutokana na upungufu wa wachezaji kwenye nafasi hiyo, ambapo alionekana kufanya vizuri muda wote wa mchezo kwa kuzuia mashambulizi ya Njombe akishirikiana vema na Abdallah Kheri, aliyeendelea kuwa katika fomu nzuri.

Mabingwa hao wana upungufu kwenye eneo hilo kufuatia mabeki wa kati, Yakubu Mohammed, Daniel Amoah na David Mwantika kuwa wagonjwa huku nahodha msaidizi Agrey Moris, akitumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano katika mchezo uliopita.

Kuelekea dakika tano za mwisho za mchezo huo, Mwamuzi, Jonesia Rukyaa, alimtoa benchini Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, akimwamuru akakae jukwaani baada ya kulalamikia baadhi ya maamuzi yake mabovu aliyokuwa akiyafanya 

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kwa siku tatu hadi Alhamisi ijayo kitakapoanza tena mazoezi kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Manungu, Turiani Morogoro Aprili 28 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Swaleh Abdallah, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Himid Mao (C), Salmin Hoza, Salum Abubakar, Frank Domayo/Mbaraka Yusuph dk 72, Bernard Arthur/Idd Kipagwile dk 50, Yahya Zayd, Ramadhan Singano/Enock Atta dk 62