MVUA kubwa inayoendelea kunyesha Mlandizi mkoani Pwani imepelekea kuahirishwa kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kati ya Ruvu Shooting na Azam FC.

Mchezo huo ulikuwa ufanyike leo saa 8.00 mchana kabla ya mvua hiyo kutibua baada ya kuanza kunyesha majira ya 7 mchana na kufanya Uwanja wa Mabatini kujaa maji kwenye eneo la kuchezea.

Baada ya mwamuzi wa mchezo huo, Shomari Lawi (Kigoma), kuzishirikisha timu zote mbili kwa kuukagua uwanja, walifikia uamuzi wa kuuharisha hadi kesho Ijumaa ukifanyika saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC kitaendelea kusalia mkoani humo hadi kitakapomaliza mchezo huo, ambao inahitaji kushinda ili kuendelea kujiweka sawa kwenye msimamo wa ligi hivi sasa ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 45.